Sunday, July 3, 2016

Unknown

Maisha ya Mbunge wa Zamani wa Temeke ( CCM ) Yapo Hatarini... Makubwa Yamkuta!

Aliyekuwa, Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abbas Mtemvu.
DAR ES SALAAM: MAISHA ya aliyekuwa, Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abbas Mtemvu, yuko hatarini, kutokana na nyumba na ofisi zake kuvamiwa mara kadhaa na watu wasiojulikana.Katika tukio lililotokea hivi karibuni, watu wasiojulikana walivamia ofisi za mwanasiasa huyo zilizopo Mtaa wa Mtukula, Temeke jijini Dar es Salaam na kupora nyaraka na mali.



Mlinzi akiwa amezirai baada ya kulishwa chakula kinachodaiwa kuwa na sumu. 
Kabla ya kufanya uporaji huo, inadaiwa watu hao walimlisha chakula kinachosadikiwa kuwa na sumu, mlinzi wa Kampuni ya Alcon Security Guard, Cornel Charles na kumfanya apoteze fahamu.
Kwa mujibu wa Mtemvu ambaye alifika eneo la tukio, watu hao walipora pikipiki tatu, viroba vya mchele, tende, mafuta pamoja na nyaraka mbalimbali muhimu.Alisema ofisi hiyo ni ya Kampuni ya Bravo Job Centre Agency Limited, inayojihusisha na utafutiaji watu ajira.Alisema, tukio hilo ni la tatu ndani ya mwaka huu ambapo Machi 5, mwaka huu , watu wasiojulikana walivamia ofisi yake iliyopo Mtaa wa Jamhuri, Posta jiijini Dar es Salaam na kupora nyaraka pekee.
“Machi 13, watu wasiojulikana walivamia ofisi zangu zilizopo Chang’ombe Temeke na kumlewesha mlinzi kwa chakula na vinywaji, ambapo walivunja ofisi na kupora nyaraka,” alisema Mtemvu.
 
Alisema, kutokea kwa tukio la juzi, kunaashiria maisha yake hayako salama na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kulifuatilia.
“Mimi naviachia vyombo vya ulinzi na usalama kuyatazama kwa umakini matukio hayo. Lazima kuna namna, kwa sababu hawa watu wanatafuta nyaraka tu,” alisema Mtemvu. 

Baadhi ya watu wa karibu wa mwanasiasa huyo, wanayahusisha matukio hayo na vuguvugu la kisiasa.
“Tangu Mtemvu aanze harakati za kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu ndani ya jimbo hili ndipo matukio yamekuwa mengi na hawa watu wanatafuta nyaraka pekee. Lazima kuna namna. Tunaomba vyombo vya usalama vichunguze kwa makini,” alieleza mtu huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake.

Hadi kufikia saa 6 mchana siku ya tukio, mlinzi huyo alikuwa amezinduka baada ya kumwagiwa maji ingawa alikuwa hajitambui, ambapo polisi kutoka Kituo cha Chang’ombe walifika eneo la tukio na kumchukua.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.