KOCHA Mkuu wa Yanga Hans Pluijm amesema amefurahi kutinga hatua ya 16 bora Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini hakufurajia na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake katika mchezo wa marudiano dhidi ya APR ya Rwanda.
Katika mchezo huo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 na kufanikiwa kufika hatua hiyo baada ya awali kuifunga APR nyumbani kwao mabao 2-1.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo Pluijm alisema kikosi chake hakikuwa na mawasiliano mazuri hali iliyowafanya wakati mwingine kutokuwa makini na kupoteza mipira ovyo.
“Nafurahi tumepita lakini ukweli sijafurahia kiwango kilichooneshwa kwani wachezaji hawakuwa makini hata kidogo, walikuwa wakipata mipira na kupoteza mapema,”alisema. Pluijm aliipongeza APR kwa kuonesha kiwango bora na kuwa na mbinu nyingi, walionesha hasira ya kutaka ushindi ndio maana walicheza kwa bidii na kuizidi Yanga.
Naye Kocha wa APR Nizah Khanfir aliipongeza Yanga kwa hatua waliyofikia na kuitakia kila la heri katika hatua inayofuata na wakati huo huo, akiitabiria kufika mbali. Baada ya Yanga kuitoa APR sasa itakutana na Al Ahly ya Misri katika mchezo ujao utakaofanyika Aprili 9.
Note: Only a member of this blog may post a comment.