Thursday, March 17, 2016

Anonymous

Mtihani No. 1 Kwa Wakuu Wapya wa Mikoa Tanzania

Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’.
Oscar Ndauka, AMANI
DAR ES SALAAM! Tayari Rais John Pombe Magufuli ‘JPM’ ameshawaapisha wakuu 26 wa mikoa yote ya Tanzania Bara, lakini kubwa ambalo ndiyo mtihani kwao ni kauli ya rais kwamba, wakapambane kuwaondoa watumishi hewa ambao wanalipwa mishahara wakati hawapo.

Kauli hiyo ya JPM imechukuliwa na wadau kama ndiyo changamoto kubwa katika halmashauri nyingi nchini ambapo katika marais wote waliomtangulia, wamekumbana na watumishi hewa kulipwa mishahara.
“Magufuli kawaambia wakuu wapya wa mikoa wakahakikishe mikoa yao haina njaa, pia amewaagiza kuhakikisha wanawasimamia watu kufanya kazi lakini mimi nasema hiyo siyo mitihani mikubwa. Suala la kuwepo kwa watumishi hewa ndiyo mtihani namba moja kwao.

“Malalamiko ya halmashauri za wilaya na miji nchini kuwa na watumishi hewa ni jipu kubwa na lililokomaa. Kama kweli watafanikiwa kupambana na watumishi hao ambao hawapo, mimi nasema nitawapa hongera kubwa,” alisema Damas Makuzi, mkazi wa Mwenge, Dar wakati akifuatilia hotuba fupi ya JPM aliyoitoa juzi, Ikulu ya Dar baada ya wakuu wa mikoa kuapishwa.
RCs (1)
Wakuu wapya wa mikoa.
Katika hotuba hiyo, JPM alitolea mfano halmashauri 14 ambapo alisema: “Mwezi Desemba mpaka Januari mwaka huu, halmashauri 14 za mikoa ya Singida na Dodoma kulipatikana kashfa ya malipo hewa ya wafanyakazi 202.
“Ni jambo la aibu kuona kila mwezi serikali imekuwa ikipoteza takribani bilioni 2.5 kutokana na malipo hewa kwa kila mkoa, natoa onyo kwa wakurugenzi wa hazina wa mikoa kuanzia sasa ikigundulika kuna malipo hewa yoyote, basi andika umeumia.”

JPM alisema kuna watumishi walioacha kazi, waliofukuzwa, waliofungwa, walio kwenye likizo bila malipo na waliofariki dunia lakini bado wanalipwa.
Pia, Rais Magufuli aliutumbua jipu mchezo wa ‘pool table’ ambao ni maarufu kwenye baa nyingi nchini. Mchezo huu umekuwa ukichezwa hata muda wa kazi, jambo ambalo rais amewaagiza wakuu hao wa mikoa kuupiga marufuku muda wa kazi kwa vile unachangia watu kutofanya kazi

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.