Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje
(pichani) anakusudia kuita mahakamani zaidi ya mashahidi 693 kupinga
ushindi wa mbunge wa sasa, Stanslaus Mabula (CCM).
Wakili wa
Wenje, Deya Outa aliieleza mahakama kuwa mashahidi hao ni pamoja na
waliokuwa wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura, wakati wa
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
“Tunatarajia kuita
mahakamani mashahidi wasiopungua 693 kuthibitisha madai yetu, kulingana
na mahitaji ya hoja tunazotaka kuzithibitisha mahakamani,” alidai wakili
Outa.
Pande zinazohusika kwenye shauri hilo namba 3 la mwaka
2015, juzi ziliweka wazi hoja wanazokubaliana na zile wanazobishania
kabla ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusulo
Sambo anayesikiliza shauri hilo kuihairisha hadi Machi 14, mwaka huu,
itakapoanza kusikilizwa mfululizo.
Pamoja na Mabula, wadaiwa
wengine katika shauri hilo linalovuta umati wa wasikilizaji ni aliyekuwa
msimamiza wa uchaguzi Nyamagana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kutokana
na wingi wa mashahidi na muda wa mwaka mmoja uliowekwa kisheria wa
mashauri ya uchaguzi kusikilizwa na kuamuliwa, wakili Outa alisema iwapo
muda huo utaisha kabla hawajamaliza kutoa ushahidi wao, wataiomba
mahakama kuwaongezea muda wa ziada.
Lembeli apeta
Aliyekuwa
mgombea ubunge wa jimbo la Kahama mjini kupitia Chadema, James Lembeli
ameruka kihunzi kingine baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Shinyanga inayosikiliza shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo
hilo kutupilia mbali pingamizi la mashahidi wa mlalamikaji lililokuwa
limewekwa na mawakili wa upande wa mshitakiwa.
Akitoa uamuzi huo
jana mjini Kahama, Jaji Moses Mzuna alisema ni kinyume cha sheria na
wala siyo haki kuzuia mashahidi wa mlalamikaji kutoa ushahidi wao, hivyo
ni vyema wakatoa na haki ikatendeka.
Uamuzi huo ulifuatia
mvutano mkali wa kisheria uliotokea Machi 4, mwaka huu, baina ya
mawakili wa upande wa utetezi na wakili wa mlalamikaji ambapo Jaji Mzuna
aliahirisha shauri hilo, hadi alipolitolea uamuzi jana asubuhi.
Katika
mvutano huo, mawakili wa utetezi Anthony Nasimire, Denis Kahangwa na
Castuce Ndamugoba walipinga mashahidi wa Lembeli kutoa ushahidi wao
kwakuwa walikiuka sheria inayowataka kuwasilisha viapo vyao mahakamani
ndani ya saa 48, kabla ya shauri kuanza kusikilizwa.
Pia Jaji
Mzuna alisema sheria hiyo ni mpya na kwamba haikujulikana kwake, kwa
mawakili wa pande zote, na hata katika rejea za kimahakama nchini ndiyo
maana hata mawakili wa utetezi wameiwasilisha wakati ushahidi
umekwishaanza kutolewa.
Alifafanua kwamba sheria ya uchaguzi inaelekeza
mlalamikaji kutoa ushahidi usioacha mianya ya mashaka, jambo ambalo pia
mahakama iliona si vyema mashahidi walioandaliwa kuzuiliwa kutoa maelezo
yao, hali itakayobana uwigo wa upatikanaji wa haki.
Kwa upande
mwingine Jaji Mzuna aliikataa hoja ya wakili wa Lembeli, Mpale Mpoki
kwamba muda wa kuandaa viapo haukuwepo kwa kuwa ilimchukua muda mwingi
kuandaa shauri hilo, ambapo Jaji Mzuna alisema haikubaliki kisheria.
Hata
hivyo alisema kuchelewa kwa Mpoki kupeleka viapo vya mashahidi hakuwezi
kuwa sababu ya Lembeli kupoteza fursa ya kudai haki yake anayohisi
alipokonywa, bali muda zaidi umetolewa wa kuandaa viapo hivyo.
Kufuatia
hali hiyo Jaji Mzuna aliahirisha shauri hilo hadi Machi 15 mwaka huu
ambapo mahakama itaanza kusikiliza maelezo ya mashahidi wa Lembeli
waliokuwa wamesubiri uamuzi dhidi ya mvutano huo wa kisheria uliopinga
mbunge huyo wa zamani wa jimbo la kahama asipeleke mashahidi wake
mahakamani.
Note: Only a member of this blog may post a comment.