WIKI iliyopita nilizungumza namna ambavyo nilishtushwa na kitendo cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ‘TCRA’ kukataza video ya wimbo wangu wa Zigo niliomshirikisha Diamond usichezwe mchana mpaka pale itakapofika saa 3 usiku na kuendelea wakati huo kuna nyimbo zingine zenye maudhui kama wimbo wangu au zaidi lakini zimeruhusiwa kwenda hewani kama kawaida…
Songa nami…
“Kitu kingine ambacho nakikumbuka katika michakato yangu ya maisha au biashara ya muziki ni siku ambayo nilienda nchini Uganda katika Jiji la Kampala, kwenye ishu moja ya muziki ambayo ilikuwa na wasanii mbalimbali wakiwemo wa Nigeria na wa nchi zingine.
“Ilikuwa ni hotelini nikiwa na mishe zangu za hapa na pale kwa mbali niliwaona wanamuziki wakubwa, Peter na Paul wanaounda Kundi la P. Square na kuiwakilisha Nigeria kimataifa, nikajipanga kuwasogelea sambamba na kutoa CD za nyimbo zangu kwani flashi sikuwa nayo. Nikaanza kuwafuata nilipowakaribia Paul mwenye rasta ndogondogo nikashangaa akiniita kwa jina AY, kiukweli nilishangaa sana kwani niliamini mimi ni mwanamuziki mchanga sana kumbe nilikuwa nafahamika.
“Nilizungumza nao na mazungumzo yangu mengi yalikuwa ni kujua ameni-fahamu vipi? Ndipo Paul aliponiambia kwamba; ‘mimi kama mfanyabiashara wa muziki ni lazima nisikilize wanamuziki wenzangu ili kuweza kujua ni namna gani muziki unaenda na unatakiwa kwenda, ni sawa na mfanya-biashara ili uweze kufanikiwa ni lazima uweze kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wenzako: “Mimi nilikufahamu kupitia mmoja wa wimbo wako unaoimba (akaimba biti ya Wimbo wa Mademu Watafutaji),” alisema Paul.
“Kiukweli jamaa huyo alinipa bonge la fundisho kubwa sana katika maisha yangu ya biashara ya muziki, huwezi amini tangu siku hiyo nimekuwa na tabia ya kusikiliza muziki wa aina mbalimba hata ninapokuwa kwenye gari naendesha huku nikiwa nasikiliza Taarab, Reggae, Dance Hall, Twist, Rock, Jazzy, Country, Kwaito, Bachata, Samba, Hip Hop, RnB, Zouk, Rhumba, Mdumange, Singeli, Segere, na zinginezo kibao.
“Hata hivyo, nawashukuru sana wasomaji wanao-fuatilia makala haya na kutoa maoni yao, yananifikia na kuyafanyia kazi akiwemo James Mtelekesya wa Mafinga ambaye yeye alinipongeza na na kunisisitizia kuwa niendelee kumtukuza na kumtegemea Mungu kwa kila jambo na pia akinitaka niwe makini katika mwanamke ninayetaka kumuoa hasa kwa kufuatilia malezi na mazingira ya mwanamke husika ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wazazi katika maamuzi hayo ya kujenga familia bora. Nami nasema asante.
“kama nilivyoanza katika simulizi hii ni ya kweli katika maisha yangu hivyo nawasihi sana tuendelee kuwa pamoja tena wiki ijayo kwa kunijua zaidi katika muziki na maisha yangu yote kwa ujumla.”
Note: Only a member of this blog may post a comment.