Na Francis Godwin, Risasi Jumamosi
IRINGA: Njemba
aliyefahamika kwa jina la Mohammed ambaye amekuwa akituhumiwa kuomba
pesa mtaani huku wakati mwingine akiwatishia watu kwa kisu pale
wanaposita kumsaidia, juzikati alikula kibano cha polisi baada kufungiwa
kazi na hatimaye kutiwa mbaroni.
Tukio la
kukamatwa kwa kijana huyo lilitokea juzikati saa 5 asubuhi, katika eneo
la Posta baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wananchi
hasa wanawake ambapo walipokuwa wakimnyima, amekuwa akiwakimbiza na kisu
mkononi.
Mmoja kati ya wanawake ambao waliwahi kutishiwa kuchomwa kisu na kijana huyo, Amina Said mkazi wa Mkwawa alisema:
“Nikajiuliza ni ombaomba kweli huyu?
Unajua Iringa ina ombaomba wengi lakini inapofikia mtu anaomba huku
akitishia kujeruhi, ni hatari sana. Yaani anaonekana ni kijana mhuni
ambaye ameamua kutumia njia hiyo haramu kujipatia pesa.”
Kufuatia
kukamatwa kwa kijana huyo, wengi walioongea na gazeti hili walisema
kuwa imekuwa afadhali kwani wamekuwa wakitembea wakiwa na hofu kubwa ya
kujeruhiwa.
“Bora polisi walivyomfungia kazi, wengi
wanamjua kijana yule kwani amekuwa akitumia njia hiyo isiyo halali
kupata pesa,” alisema Salum Mikidadi mmoja wa wafanyabiashara ndogondogo
eneo la Posta.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Peter
Kakamba, mbali na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo pia
aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wanapoona
matukio ya watu kama hao kwani ni hatari katika jamii.

Note: Only a member of this blog may post a comment.