
Nafahamu fika kuwa kwenye kila matokeo makubwa na muhimu kama hayo wapo wahitimu ambao wameanguka vibaya kwa kufeli na wengine waliokuwa na furaha ya kufaulu vizuri.
Wanafunzi makini hutakiwa kujifunza kupitia hali hizi mbili, kwa namna moja au nyingine na wao wataifikia steji hiyo katika kipindi cha masomo yao ambapo watatakiwa kusubiri na kupokea matokeo muhimu hasa ya mitihani ya mwisho ambayo wameifanya.
Ni wazi kuwa wanafunzi wengi kwa nyakati tofauti wameshapitia hatua hii na wanajua changamoto zake hasa pale wanapokuwa wamefeli, vilevile wanafunzi wanafahamu jinsi furaha inavyokuwa pindi wanapokuwa wamefaulu.
Kwa namna yoyote ile mwishowe utagundua kuwa unachotakiwa ni kusoma tu ili kusonga mbele kwa kuwa hisia za kufeli huumiza zaidi na sidhani kama kuna mwanafunzi mwenye malengo ambaye angependa kukutwa na hali hiyo katika kipindi cha kujifunza kwake.
Kwa machache hayo, nitangulize pole kwa wahitimu wote wa kidato cha nne ambao wameanguka hali kadhalika niwape pongezi wale ambao wamefaulu na kati yao wale waliokuwa wakiwasiliana na mimi moja kwa moja kwa ushauri wa mara kwa mara hasa katika kuwaongezea mbinu za kusoma na kufaulu.

Note: Only a member of this blog may post a comment.