Mtoto huyo baada ya kuokolewa na wasamalia wema.
Shekidele, Risasi
MOROGORO: Mwanamke aliyefahamika
kama Mama Gladnes, ambaye ni mchepuko wa mtu aliyefahamika kwa jina la
Yusuf, Jumamosi iliyopita alimbwagia mtoto mwanaume huyo baada ya
kusitishiwa huduma ya malezi, tukio lililotokea huko Nanenane Tubutu,
mjini Morogoro.
Baadhi ya wapangaji wa nyumba anayoishi
Yusuf waliliambia gazeti hili kuwa saa 2 usiku, walisikia zogo likitokea
katika chumba cha mwenzao na walipokwenda kuangalia kulikoni, wakabaini
uwepo wa mama Gladnes aliyekuja kudai matunzo ya mtoto huyo, lakini
mwanaume akimkana kuwa siyo mwanaye maana hafanani naye.
“Kusikia
hivyo, mama Gladnes alikuja juu na kwa hasira akatoka nje akisema
anarudi kwao Kigoma hivyo hawezi kwenda na mtoto wa mtu, akaenda kumtupa
mtoto huyo kwenye kichaka kisha akapanda pikipiki iliyomleta na
kutokomea.
“Kwa kuwa tunafahamu eneo hilo lina Mbwa
wakali nyakati hizo za usiku, mke wangu na jirani Upendo tuliamua
kwenda kumuokota mtoto huyo na kulala naye ambapo muda huu tunajiandaa
kumpeleka polisi,” alisema mmoja wa wapangaji hao aliyejitambulisha kama
Lukinga.
Akihojiwa na gazeti hili, Yusuf alikiri
kutokea kwa tukio hilo na kufafanua kuwa mtoto huyo ni wake, lakini
alimkataa kwa vile mama Gladnes alikiuka makubaliano yao, ambayo
yalikuwa jambo hilo liwe siri isiyojulikana kwa familia yake.
Habari zilizopatikana baadaye zilisema
wawili hao walikwenda kituo cha polisi na kukutanishwa katika dawati la
jinsia, ambako walikubaliana kuwa mwanaume huyo awe anampatia mzazi
mwenzake kiasi cha shilingi elfu sitini kila mwezi, kama matunzo kwa
mtoto huyo, jambo ambalo lilikubaliwa na wazazi wote.
Afisa mmoja wa polisi aliyezungumza kwa
sharti la kutotaja jina kwa kuwa siyo msemaji, alithibitisha kufikiwa
kwa makubaliano hayo na kwamba mwanamke huyo amekubali kumchukua na
kuendelea kumlea mwanaye ilimradi tu apewe kiasi hicho cha fedha
kilichokubaliwa.

Note: Only a member of this blog may post a comment.