Mchungaji Patrick Mgaya (pichani) ambaye
alikuwa na Mchungaji Christophar Mtikila siku anapatwa na mauti kutokana
na ajali ya gari mkoani Pwani wakitokea Njombe kuelekea jijini Dar,
amefikishwa katika Kituo cha Polisi, Njombe, Uwazi limenasa.
Kwa mjibu wa mke wa marehemu Mtikila, Georgia, Mchungaji Mgaya
amefikishwa polisi na watu wengine kwa madai kuwa wamezuia vyombo vya
muziki vilivyokuwa vikitumika katika kampeni za siasa za Democratic
Party (DP) ambavyo walikuwa wameviazima kutoka kanisani kwao marehemu.
Mama Georgia alisema kwamba walifungua mashtaka polisi Novemba 3,
mwaka huu na shauri hilo likapewa jalada namba NJ/RB/3009/2015 katika
Kituo cha Polisi Njombe na tayari Mchungaji Mgaya na wenzake
wameshahojiwa kuhusiana na sakata hilo.
“Mchungaji Mgaya ndiye aliyepewa hivyo vyombo na marehemu Mtikila
kupeleka Njombe kwa ajili ya kampeni kipindi hicho kabla ya uchaguzi na
ni vya Kanisa la Full Salvation ambalo Mchungaji Mtikila alikuwa
kiongozi wake mkuu, akaamua kuazimisha kwa chama kwa ajili ya kufanyia
kampeni.
“Nashangaa kwa sasa Mgaya anasema kwamba vyombo ni vyake na kuwa yeye
ndiye aliyevinunua hivyo hawezi akavikabidhi kwa mtu yeyote kitu
ambacho si kweli, najua haki itatendeka, nawategemea polisi kufanya
uchunguzi wa kina na kila kitu kitajulikana,” alisema mama huyo huku
machozi yakimbubujika.
Mchungaji Mgaya alipoulizwa juu ya sakata hilo kwa njia ya simu juzi
Jumapili alikiri kufahamu suala hilo na akasema suala hilo amemuachia
Mungu.
“Tena basi suala hilo nimeshalimaliza polisi Njombe sasa sipendi kabisa kulizungumzia tena,” alisema Mchungaji Mgaya.

Note: Only a member of this blog may post a comment.