Rais Dk. John Magufuli, amesema
 hakuna mfanyabiashara aliyemchangia  kumuwezesha kuingia Ikulu katika 
kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, ili aweze kusimamia 
ipasavyo makusanyo ya kodi kwa faida ya wananchi.
Dk.
 Magufuli alitoa kauli hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati 
akizungumza na wafanyabiashara na wawekezaji wa sekta binafsi, katika 
kikao cha pamoja kilichoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania 
(TPSF) na Baraza la Biashara la Taifa ( TNBC) kwa ajili ya kufahamiana.
Alisema
 wakati wa kampeni hadi kufikia siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka 
huu, hakupokea senti yoyote kutoka kwa wafanyabiashara kwa kuwa alijua 
akiingia madarakani anakwenda kufanya kazi tu.
“Nilijiepusha
 na fedha, mchango wowote kutoka kwa wafanyabiashara, kama yupo 
mfanyabiashara yeyote alinichangia hata shilingi mbili asimame hapa 
aseme, nilikwepa kwa sababu nilitaka iwe kazi tu,” alisema.
Rais
 Magufuli aliwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kuweka mbele 
maslahi ya umma, ili kuwasaidia wananchi wanyonge badala ya kushirikia 
kuwakandamiza.
Alisema Tanzania ni tajiri na ina rasilimali nyingi, lakini kinachokosekana ni kushindwa kuweka mbele maslahi ya umma
Alisema
 anatambua sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa katika kujenga uchumi na 
kazi kubwa ya serikali katika uchumi wa soko ni kujenga mazingira mazuri
 kwa sekta binafsi.
“Napenda
 kuwahakikishia kuwa serikali ya awamu ya tano itajenga mazingira mazuri
 zaidi kwa ajili ya ustawi wa sekta binafsi, nitapunguza na kuondoa 
vikwanzo na urasimu unaokwamisha uwekezaji wa biashara nchini,” alisema.
Rais
 Magufuli pia alisema ataangalia uwezekano wa kupunguza utitiri wa kodi 
na ushuru ambao umekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara na wananchi.
Alirejelea
 mfano wa mkoa wa Kilimanjaro na Kagera wakati wa kampeni alipewa kilio 
cha wakulima wa zao la kahawa kutozwa kodi zaidi ya 26 na kusababisha 
kusafirisha kwa njia ya magendo kwenda Uganda.
“Soko
 la kahawa duniani ni lilelile, lakini Uganda hawana kodi hizi, biashara
 nyingine ni biashara ya sukari, tukiungana pamoja na kufanya kazi 
pamoja kwa kuweka mbele maslahi ya taifa nchi hii itaendelea,” alisema.
Akizungumzia
 sekta ya Benki, Rais alisema anafahamu kuwa Tanzania kuna benki 54 
ambazo zote zinafanya biashara na serikali lakini hazijajikita maeneo ya
 vijijini ambako ndiko kuna wananchi.
“Nimefanya
 uchambuzi fedha zilizowekwa na mashirika ya umma ambazo ni fedha za 
serikali ni zaidi ya Sh. bilioni 550, benki zinachukua kiasi cha fedha 
na kwenda kuziweka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hapa inakuwa benki 
inafanyabiashara na serikali kwa kutumia fedha za serikali, hivyo ni 
sawa na serikali kufanya biashara kwa fedha zake,” alisema.
Rais alisema mashirika mengine yamewekeza fedha kwenye benki hizo na hazizalishi riba yoyote.
Kuhusu sekta ya viwanda,Dr. Magufuli alisema
 inashangaza kuona Tanzania ina mifugo mingi inayoweza kuzalisha ngozi 
kwa wingi lakini hakuna viwanda vya ngozi vinavyozalisha na kutengeneza 
viatu inashindwa na Ethiopia ambayo haina ngozi.
“Kuna
 umuhimu gani viatu vya kuvaliwa na wanajeshi, wananchi na hata sisi 
tuagize kwa nchi ambazo hazina ng’ombe, unajua wenzetu wanatucheka sana 
na kutuona hatufai,” alisema.
Alisema
 vipo viwanda vilivyobinafsishwa na vingine vimegeuzwa sehemu ya 
kuhifadhi mifugo, huku akitolea mfano wa mji wa Morogoro ambao ulikuwa 
mji wa viwanda lakini kwa sasa vyote vimekufa.
“Mfano
 mkoani Arusha kuna kiwanda kinakusanya maziwa ya ng’ombe kutoka kwa 
wafugaji, lakini yanapelekwa Kenya kuyahifadhi kwenye vifungashio na 
kuyarudisha nchini kuuza, ingewezekana kabisa kufungashia nchini na 
kuuza,’ alisema na kuongeza:
“Serikali
 tupo, sekta binafsi tupo, TNBC wapo, makatibu wakuu wapo, wawaziri wapo
 na rais nipo. Nazungumza hivi siyo kwamba nafurahi, inasikitisha, 
nazungumza haya kwa kuwa najua hakuna Tanzania kama hakuna nyinyi,” alisema.
Akizungumzia
 sekta ya utaliii,Rais alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii 
ambavyo vinaweza kuliingizia taifa fedha nyingi, lakini kuna ujanja 
mwingi ikiwamo wageni kulipa fedha kwenye nchi zao na kuja nchini 
kutalii, jambo ambalo linaikosesha serikali mapato.
“Unaweza
 kusema watalii milioni 1.1 wameingia nchini na kujiwekea malengo ya 
watalii milioni mbili, tujiulize wanaingiza shilingi ngapi, wanalipia 
nchini au kwao, wanaweza kuacha fedha kwao alafu nyie mnakuja kuona sura
 zao na kuhesabu idadi, ni afadhali wakaja watano lakini tukapata fedha 
nyingi,” alisema. 
Alisema ni lazima kujiuliza kwanini Misri inapata watalii wengi na haina vivutio vingi kama Tanzania, hivyo ni lazima vikwazo vyote vikaondolewa nchini.
Alisema ni lazima kujiuliza kwanini Misri inapata watalii wengi na haina vivutio vingi kama Tanzania, hivyo ni lazima vikwazo vyote vikaondolewa nchini.
Aidha,
 Rais aliwataka wafanyabiashara hao kujenga viwanda vya kusindika samaki
 katika ukanda wa kusini, kwa kuwa kuna eneo la kutosha kwa ajili ya 
kazi hiyo.
Alisema
 Bahari Kuu kuna raia wa nje wanaendesha uvuvi haramu na wana meli kubwa
 zenye viwanda vya kusindika samaki ambazo husafirishwa kwenda nje moja 
kwa moja, jambo ambalo linaweza kufanywa na wafanyabiashara au 
wawekezaji wa Tanzania.
Rais
 alisema amechoka kuona Tanzania inachezewa na kugeuzwa shamba la bibi 
na wafanyabiashara wake wakidharauliwa mbele ya nchi nyingine na kwamba 
wakati umefika wa kuwekeza ili kujenga heshima ya nchi na kukuza uchumi 
wa Taifa.


Note: Only a member of this blog may post a comment.