Sunday, November 8, 2015

Anonymous

YANGA SC Yaonesha JEURI YA FEDHA!

Ni fedha juu ya fedha! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na Yanga kuhitaji fungu kubwa la Sh. bilioni 1.3 ili kumwachia mshambuliaji wake asiyezuilika Donald Ngoma.

Siku moja baada ya kuweka wazi kuwa uko tayari kumuuza Mzimbabwe huyo pamoja na nyota wake wengine wa kimataifa; Andrey Coutinho na Vincent Bossou, uongozi wa Wanajangwani sasa umeweka wazi bei ya mkali huyo wa magoli (Ngoma).

Jana Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha, aliiambia NIPASHE Jumapili kuwa klabu hiyo ipo tayari kumuachia Ngoma kwa gharama ya dola 600,000 ambazo ni zaidi ya Sh. bilioni 1.3 za Tanzania, ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 1.2 kulinganishwa na Sh. milioni 97 walizomunua kutoka FC Platinum ya Zimbabwe.

"Yanga inahitaji dola 'laki sita' tu ili imuachie Ngoma, vinginevyo hatauzwa kokote. Klabu iliyoleta ofa ni ya Afrika Kusini, lakini nayo bado ni kidogo. Tunaangalia iwapo wataweza kufika dau tunalolitaka," alisema.
Hata hivyo, Tiboroha hakuwa tayari kuweka wazi jina la klabu hiyo ya 'Sauzi' iliyowapa ofa ya kumsajili nyota huyo.
"Tukiuza mchezaji, tunataka tupate fedha ya kutosha ambayo na sisi tutaingia sokoni kusaka mchezaji mwenye uwezo sawa au zaidi ya mchezaji atakayekuwa ameuza," alieleza zaidi Tiboroha.

Ngoma (26) amekuwa na msaada mkubwa katika kikosi cha kocha mkuu Mdachi Hans van der Pluijm cha Yanga tangu asajiliwe msimu huu akifunga mabao nane Ligi Kuu, moja nyuma ya kinara Elias Maguli wa Stand United.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.