Kikwete,
ambaye alikuwa amevalia suti maarufu kama ‘kaunda suti’ yenye rangi
nyeusi, alionekana akiingia katika viunga vya Mlimani City saa 5:00.
Mwandishi wetu ambaye alikuwepo katika viunga hivyo vya Mlimani City alishuhudia Kikwete akiwasili katika maeneo hayo akiwa katika msafara wa magari manne na pikipiki moja.
Rais
huyo mstaafu pia alikuwa ameambatana na mkewe, Salma Kikwete, aliyekuwa
amevalia mavazi ya kitenge pamoja na walinzi wao wanne.
Hatua hiyo ilionekana kushangaza baadhi ya watu waliokuwepo katika maeneo hayo, huku wengi wao wakionekana kutaka kumsalimia.
Mwandishi wetu ambaye muda wote alikuwa akimfuatilia Rais Kikwete na mke wake, alishuhudia
wakiingia katika maduka ya Game na kufanya manunuzi kwa dakika
zisizopungua 10 hadi 15 na baadaye kutoka nje na walinzi wake
wakionekana kubeba mifuko iliyokuwa na bidhaa walizonunua.
Kama
ilivyo hulka ya Rais Kikwete alipotoka nje ya duka hilo alianza
kusalimiana na mtu mmoja ambaye alionekana kufahamiana naye.
Hatua hiyo ilimpa fursa ya kuwasalimia watu wengine waliokuwa karibu na tawi la benki moja.
Baada ya hapo msafara wake uliondoka na kuelekea Barabara ya Sam Nujoma.
Tangu
achaguliwe kuwa rais mwaka 2005 itifaki na majukumu yake ya urais
yalikuwa yakimbana Rais Kikwete na hivyo kushindwa mambo yake binafsi
kama walivyo raia wengine.
Pamoja
na kwamba Kikwete sasa ni raia, lakini kutokana na wadhifa aliowahi
kuushika wa urais bado halingani na raia wengine wa kawaida, ingawaje
majukumu ya urais yamepungua na hivyo kumpa fursa ya kutembea katika
maeneo ya wazi na kufanya matumizi ya kawaida kama alivyofanya jana.
Tangu
alipoachia kiti cha urais na kumkabidhi Dk. John Magufuli baada ya
kuapishwa Novemba 5, Kikwete amekuwa akiishi nyumbani kwake Msoga,
mkoani Pwani.
Rais Kikwete aliondoka rasmi Ikulu na familia yake Ijumaa iliyopita Novemba 6 na kuanza maisha mapya kijijini kwake huko.
Credit: Mtanzania
Note: Only a member of this blog may post a comment.