Sunday, November 22, 2015

Anonymous

Raia wa Uingereza Akamatwa na Madawa ya Kulevya Uwanja wa Ndege (JNIA) Jijini Dar

Jeshi la Polisi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), limemkamata raia wa Uingereza, Faiz Abdullah Ali (55) kwa tuhuma za kukutwa na kilo 22 za dawa za kulevya aina ya mirungi ikiwa imefungwa kwenye kanga na kuhifadhiwa ndani ya mabegi mawili.

Mirungi hiyo imekamatwa siku nne baada ya watu wawili kutiwa mbaroni uwanjani hapo, wakiwa na kobe hai 201 wenye thamani ya Sh30.4 milioni kwenye boksi, wakisafirishwa kwenda Kuala Lumpa, Malaysia.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Martin Otieno alidai jana kuwa mtuhumiwa huyo, mwenye asili ya Somalia, alikamatwa juzi saa 3.40 usiku katika eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria akiwa na mirungi hiyo.

Otieno alisema polisi wa JNIA kwa kushirikiana na kikosi cha kazi, walitilia shaka mabegi hayo ya mtuhumiwa huyo, mzaliwa wa Kismayu, Somalia kabla ya kusafirishwa kwa ndege ya Shirika la Emirates kuelekea London Uingereza kupitia Dubai.

“Mirungi hiyo ilikuwa imefungwa kwenye kanga na kuwekwa kwenye mabegi mawili moja la rangi ya silver na jingine jeusi ili mashine ya ukaguzi isitambue kilichomo ndani, lakini kutokana na mashine hizo kuwa za kisasa ilionyesha kilichomo ndani kuwa ni mirungi.

“Kama mtu anataka kusafirisha mirungi kwenye ndege anaweza kuhatarisha maisha ya wananchi ,” alisema Otieno. Alisema walipokagua hati ya kusafiria ya mtuhumiwa huyo, ilionyesha kuwa aliingia nchini Novemba 10.

Alisema taarifa zaidi zinaonyesha kuwa mtuhumiwa huyo aliwahi kuingia nchini Julai 20 na kukaa kwa siku tano na kwamba polisi wanafuatilia shughuli alizokuwa akifanya kwa kipindi hicho.

Otieno alisema mtuhumiwa huyo alipohojiwa alidai kuwa aliwasili nchini kwa ajili ya kufanya utalii. Hata hivyo, alisema wanaendelea kumhoji na kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini washirika wake.

Kumekuwa na jitihada za Serikali kupambana na biashara haramu za dawa hizo huku wadau wakitaja rushwa na wanasiasa kuwa ndivyo vinavyochangia kukithiri kwa biashara hiyo kwa miaka ya hivi karibuni.

Serikali iliwasilisha muswada wa kupinga dawa ya kulevya bungeni Machi mwaka huu kwa lengo la kupambana na biashara hiyo nchini.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.