LEO
ni siku muhimu sana katika mstakabali stahiki wa nguvu ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo wabunge mnaamua nani awe
kiongozi wa vikao vyenu, kwa ngazi za spika, naibu wake na wenyeviti.
Kila chama kimetoa majina ya wawakilishi wao katika kinyang’anyiro hicho cha nafasi muhimu sana bungeni. Kura zenu ndizo zitaamua nani akalie kiti hicho.
Hapa nataka nitete kidogo nanyi wawakilishi wa wananchi ambao mmechanganyika kuna wanasheria, walimu, mainjinia na wana taaluma mbalimbali.
Ni wazi kwamba, chombo chenu (bunge) ni mhimili muhimu katika kusimamia, kushauri na wakati mwingine kushurutisha serikali kutimiza wajibu wake kwa wananchi. Kwa maana nyingine, mnabeba asilimia nyingi sana katika ufanisi wa maisha bora kwa Watanzania.
Pamoja na hayo, bado bunge halitakuwa na maana tena endapo viongozi wake, kwa maana ya spika, naibu spika na wenyeviti watakuwa watu wasiojali masilahi ya taifa.
Namaanisha kama spika, naibu wake au mwenyekiti atakuwa ni mtu wa kuzima hoja za msingi kwa taifa, kuwa na upendeleo kwa wabunge kuchangia hoja, hakika bila kutafuna maneno litakuwa bunge lisilokuwa na makali yanayotarajiwa na wapiga kura.
Ni wazi kuwa, uchaguzi wa mwaka huu umeingiza vijana wengi bungeni, hivyo wapiga kura wanatarajia kuwa na bunge la nguvu na lenye tija kwa taifa katika kuisimamia vyema serikali.
Ujumbe wangu kwenu wabunge, tumieni busara, hekima na usomi wenu katika uchaguzi huu kumpata spika ambaye hatajali masilahi ya chama chake linapokuja suala la mijadala muhimu yenye manufaa kwa taifa, ni lazima awe spika, naibu au mwenyekiti asiyekuwa na ‘unazi’ na chama chake, si mtu wa kutumiwa na serikali kuzima baadhi ya hoja nzito zinazotetea mambo nyeti ya wananchi.
Tayari mnawafahamu wagombea, baadhi yao mnawajua vyema, tafadhalini sana, wapimeni kwa vigezo muhimu na kwa sifa stahiki ambazo kwa pamoja mnaamini watakuwa viongozi wa bunge wanaojua vyema kutenganisha mihimili mitatu, serikali, bunge na mahakama.
Tena, katika uchaguzi wa mwaka huu wa spika na jopo lake, nawaomba wabunge wekeni pembeni itikadi za vyama vyenu na badala yake mchague watu ambao linapokuja suala la kujadili mambo muhimu, wawe tayari kusimamia kwa weledi jambo hilo na kuzima na kutoondoa hoja muhimu kama tulivyoshuhudia kwa baadhi ya vikao vilivyopita.
Nijuavyo, masilahi ya taifa, hayajali chama, mambo muhimu lazima yajadiliwe kwa kina na kwa hoja zenye mashiko ili kuondoa ukiritimba ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya viongozi.
Hapa, naomba niwe mkweli kuwa, bunge lililoisha, hakika lilipoteza hadhi yake, lilipoteza imani kwa wananchi kutokana na baadhi ya hoja muhimu kuzimwa na kunyimwa fursa kwa baadhi ya wabunge wa upinzani kujadili na kuchangia mijadala nyeti.
Bunge lile pia lilitoa maazimio kwa serikali lakini baadhi yalipuuzwa na hatukusikia hatua zikichukuliwa.
Hatutarajii kuona mambo kama hayo yakijirudia tena katika bunge hili ambalo watu wengi hususan vijana wana imani nalo kutokana na aina ya wabunge wapya waliochaguliwa na hata kwa baadhi ya wenyeji.
Imani yangu ni kuwa mtamchagua spika, naibu spika na mwenyekiti ambaye ana vigezo na sifa mahususi katika kuongoza vikao vya bunge kwa weledi mkubwa na uliotukuka.
Nawatakieni uchaguzi mwema kwa spika na jopo lake zima, zingatieni niliyoainisha hapo juu, kila la heri na Mungu awatangulie katika mbio zenu za kumpata spika stahiki. Naomba kuwasilisha.
Note: Only a member of this blog may post a comment.