Monday, November 16, 2015

Anonymous

Historia Mpya Kuandikwa Dodoma Wiki Hii...Spika wa Bunge, Waziri Mkuu wa 11 wa Bunge la 11 Kujulikana Wiki Hii!

Historia mpya inaandikwa wiki hii mkoani Dodoma ambako Bunge la 11 la Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli linatarajiwa kuanza vikao vyake kesho.

Wiki hii Watanzania watashuhudia upatikanaji wa Spika mpya pamoja na Naibu wake, na pia ni mwanzo wa mikutano ya Bunge jipya, lakini pia ni wiki ambayo Bunge litathibitisha jina la Waziri Mkuu wa 11 wa Tanzania ambaye kwa vyovyote atakuwa ni mpya.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, kuanzia Ijumaa hadi jana ilikuwa usajili kwa wabunge wote wanaotarajiwa kushiriki Bunge hilo na leo kuanzia saa nne asubuhi hadi saa sita mchana, itakuwa kikao kwa wabunge wote na kisha watatembelea Ukumbi wa Bunge.

Ratiba inaonesha kuwa alasiri kutakuwa na mikutano ya kamati za vyama na hiyo itakuwa mahususi kwa ajili ya kuchagua mgombea Uspika kupitia chama husika.

Kesho Jumanne itakuwa ni kuanza kikao cha kwanza cha Bunge na kusomwa Tangazo la Rais la kuitisha Bunge ambapo pia kutafanyika uchaguzi wa Spika na kisha ataapishwa.

Baada ya tukio hilo, utapigwa Wimbo wa Taifa na baadaye wabunge wataanza kuapishwa shughuli itakayoenda hadi Alhamisi asubuhi.

Alhamisi jioni itakuwa kuthibitisha jina la Waziri Mkuu ambapo Spika atakuwa amepokea jina hilo kutoka kwa Dk Magufuli na baadaye kutafanyika uchaguzi wa Naibu Spika.

Mawaziri wakuu 10 waliopita ni Mwalimu Julius Nyerere, Rashidi Kawawa, Edward Sokoine (wote marehemu), Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, Joseph Warioba, John Malecela, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Mizengo Pinda.

Ratiba inaonesha Ijumaa alasiri Rais Magufuli atahutubia Bunge na baadaye itatolewa hoja ya kuahirisha Mkutano huo wa Kwanza wa Bunge la 11.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.