Mwanamuziki wa Hip Hop kutoka nchini Marekani, 50 Cent.
WALE wanaopenda muziki wa Hip Hop au wanaofuatilia
showbiz ya kimataifa wanafahamu vizuri jinsi 50 Cent alivyo na ‘sinema’
nyingi katika maisha yake.
Moja kati ya mijengo anayomiliki 50 Cent.
50 Cent ambaye alikulia katika maisha ya kifukara kabla ya kupata
utajiri mkubwa, amekuwa ni mtu wa kutawala katika vyombo vya habari kwa
mambo tofauti, ikiwemo bifu, kutambia utajiri, lakini yote kwa yote
anajua jinsi ya kupambana kuzitafuta fedha.
Awali ilijulikana 50 Cent ambaye jina lake kamili ni Curtis Jackson
ana utajiri mkubwa, ghafla akatangaza kuwa amefilisika na anauza vitu
vyake vingi vya thamani.Wakati akitangaza hivyo, siku chache baadaye
akaonekana akionyesha nyumba kubwa ya kifahari aliyodai ni yake na
anaijenga katika Bara la Afrika, pia alionekana sehemu tofauti za
starehe akijiachia na kutumia fedha nyingi.
Kitendo cha kujitangaza kuwa amefilisika ilionekana ni ujanja wa
kutaka kukwepa adhabu ya mahakama ambayo ilimtaka amlipe mwanamama
Lastonia Leviston dola milioni 5 (Sh bilioni 10) kutokana na kuvujisha
video yake ya ngono kwenye mitandao.
Leviston, 36, ambaye ni mzazi mwenza wa Rick Ross alishinda kesi na
hivyo kutakiwa kulipwa fedha hizo, ukumbuke kuwa Rick Ross na 50 Cent
hawana uhusiano mzuri.Wakati ikionekana anafanya maigizo, sasa 50 Cent
ambaye aliingiza fedha nyingi zaidi mara baada ya kutoa albamu yake ya
Get Rich Or Die Tryin mwaka 2003 ametangaza kuiuza nyumba yake yenye
thamani kubwa.
Nyumba hiyo yenye vyumba vya kulala 21 na mabafu 25, haikupata mteja
kwa bei hiyo, imeingizwa sokoni tena kwa dola milioni 8.5 (Sh bilioni
17). Mwanasheria wa 50 Cent amedai mteja wake anataka kuiuza ili apate
fedha za kulipa deni analodaiwa.
Mwanasheria huyo amesema sababu nyingine ya kuweka sokoni mjengo huo
ambao umo ndani ya eneo analomiliki lenye ukubwa wa eka 17, ni gharama
zake za kawaida kumshinda 50 Cent, anadai kuifanya nyumba hiyo iwe
katika ubora wake gharama zake ni dola 72,000 (Sh milioni 144) kwa mwezi
na pia kutunza bustani zote ni dola 5,000 (Sh milioni 10) kwa mwezi.
Ndani ya nyumba hiyo kuna ukumbi, casino, gym, jumla kuna vyumba 52,
majiko tisa na ukumbi wa sinema. Bado haieleweki vizuri kama madai hayo
ni ya kufilisika ni ya kweli.
Wakati huohuo, mwanasheria huyo amesema kuwa Benki ya Sun Trust inamdai 50 Cent, 40, dola milioni 4 (Sh bilioni 8) ambazo alikopa kwa ajili ya kampuni yake ya kupromoti mchezo wa ndondi.
Sheria ya mtandao ya kuwashitaki wanaovuruga mambo katika mitandao,
ndiyo imeanza kutumika Tanzania, hivi karibuni, mkasa huu unaweza kuwa
darasa kwao. Kwani 50 Cent aliona ufahari kusambaza video hiyo ambayo
imemtokea puani.

Note: Only a member of this blog may post a comment.