Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma.
Ibrahim Mussa na Mohammed MdoseLICHA ya kufunga bao la ushindi katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma amewalaumu mabeki wa Mtibwa waliokuwa wakiongozwa na Salim Mbonde, kutokana na kumchezea kibabe na kumpiga rafu za makusudi.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Ngoma kucheza nje ya Dar katika ligi kuu, alisema alishindwa kucheza vizuri kutokana na mabeki hao kumpania na kumchezea vibaya.
“Uwanja tuliochezea kwa kweli ni mbovu hasa sehemu ya kuchezea (pitch), ilikuwa ikinipa shida mwanzoni lakini nilijitahidi kuizoea.
“Mabeki wa Mtibwa nao walifanya mambo mengi ili wanitoe mchezoni lakini ilishindikana kwa kuwa nilitambua umuhimu wa mchezo na sikutaka kuwaangusha mashabiki ambao wamesafiri kutoka sehemu mbalimbali mpaka hapa (Morogoro) kuja kutupa sapoti.
“Lakini siyo kwamba wapinzani walikuwa wabaya, isipokuwa mabeki wao walionekana kutukamia na mara kadhaa wameniangusha kwa kunicheza faulo za makusudi lakini kizuri ni kuwa tumeshinda,” alisema Ngoma ambaye mpaka sasa amefunga mabao manne katika ligi kuu.

Note: Only a member of this blog may post a comment.