Stori: Na Brighton Masalu
MAMBO yameiva!
Nyota wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ (20) yu
mbioni kupanda tena Kizimba cha Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es
Salaam kwa ishu yake ile ya madai ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa
msanii wa filamu nchini, marehemu Steven Charles Kanumba ‘The Great’,
Amani lina ripoti mkononi.
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka ndani
ya mahakama hiyo jijini Dar, kesi hiyo ilisimama kwa muda wa mwaka mmoja
na zaidi kutokana na matatizo yaliyo nje ya uwezo wa mahakama, lakini
sasa matatizo hayo yameisha hivyo kesi hiyo itaanza kurindima siku
yoyote kuanzia sasa.
NI BAADA YA MWAKA MMOJA NA MIEZI NANE
Tangu kusimama kwa kesi hiyo, mwaka
2013, ilitarajiwa kuanza tena kusikilizwa Februari 17, 2014 lakini
ikakwama kutokana na matatizo mbalimbali ya kimahakama.
ITAANZA UPYA
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu,
mwendesha mashtaka wa serikali atamsomea mashtaka upya Lulu lakini neno
la msingi kwenye mashtaka hayo ni; mnamo Aprili 7, 2012 anadaiwa kumuua
bila kukusudia, Steven Kanumba.
“Baada ya kuulizwa, Lulu akiwa kama
Elizabeth Michael atajibu anachotaka kutoka moyoni kulingana na ukweli
anaoujua kisha jaji atampangia tarehe ya kurudi tena,” alisema mtoa
habari huyo.
MAHAKAMA ITATUMIA MWONGOZO WA JAJI MKUU
Tofauti na madai ya awali kwamba, kesi
hiyo ingeendeshwa kwa siku 730, habari za uhakika zinasema kuwa, kesi
itakapoanza safari hii haitasimamishwa mpaka siku ya hukumu. Kwa hiyo
itategemea na kasi ya hakimu husika.
“Lakini pia, kauli ya Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mohamed Chande Othman anayoitoa kila Siku ya Sheria Duniani
(Februari 3) kwamba kesi zote za jinai zisipitishe miaka miwili,
itazingatiwa,” kilisema chanzo.
Kikaongeza: “Lakini nadhani ikianza
safari mwaka huu, naamini mpaka mwaka 2017 itakuwa imemalizika kama
sheria ya miaka miwili itazingatiwa.”
Chanzo hicho kilisema kuwa, bado mcheza
sinema maarufu Bongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ anaendelea kutambulika
na mahakama kama mdhamini wa Lulu. Kwa hiyo, anatakiwa kuendelea na
jukumu la kumlinda Lulu ili asiruke dhamana (asitoroke, asikiuke
masharti ya dhamana).
MASHAHIDI WAJIPANGE
Chanzo kilisema baadhi ya mashahidi muhimu nao watapewa taarifa ya kimaandishi ili tarahe ya kesi wafike mahakamani.
Mashahidi hao ni Dokta Kidume ambaye
alikuwa akimtibu Kanumba pia ndiye alikuwa mtu wa pili kufika kwenye
chumba cha marehemu mara baada ya kuanguka na kupoteza maisha.
Seth Bosco naye anatakiwa kujiandaa
kupokea wito huo kwani yeye siku ya tukio alikuwa nyumba moja na
marehemu (vyumba tofauti). Yeye alimshuhudia Kanumba akiwa katika hali
mbaya baada ya kutoelewana na Lulu na kukimbia kwenda kumwita Dokta
Kidume.
WAKILI WA LULU AZUNGUMZA
Peter Kibatala ni wakili maarufu jijini Dar. Yeye ndiye mwanasheria katika kesi ya Lulu. Amani lilimtafuta ili kujua hatima ya kesi hiyo na madai kwamba iko njiani kuanza upya. Alisema:
“Aaa! Sijajua. Lakini kwa kawaida
mahakama itakapoona mambo yameanza, kesi inatakiwa kuanza kusikilizwa
itatakiwa kutoa taarifa siku sita kabla.”
AMZUNGUMZIA LULU
Wakili Kibatala alikwenda mbele zaidi
kwa kusema kuwa, mteja wake (Lulu) amekuwa akimpigia simu mara kwa mara
akitaka kujua tarehe ya kesi yake kuanza tena.
“Hata Lulu mwenyewe amekuwa akinipigia
simu kuulizia ni tarehe ngapi kesi yake itaanza tena. Nitapewa taarifa
siku sita kabla,” alisema mwanasheria huyo.
LULU PRESHA INAPANDA
Naye rafiki wa karibu wa Lulu, akizungumza na gazeti hili huku akiomba hifadhi ya jina lake, alisema:
“Ninyi mnaandika Lulu siku hizi
anakunywa sana pombe. Mnajua hayuko sawasawa. Ile kesi yake ya kumuua
(bila kukusudia) Kanumba inamtesa sana kichwani.
“Ukimya wa kesi unamfanya ashindwe kujua
hatima yake. Kila akikumbuka anampigia simu wakili wake. Mbaya zaidi
kuna watu wanamwambia kesi inaweza kukaa kimya kwa muda mrefu halafu
siku moja ikalipuka na kuwa nzito. Kwa hiyo wakati mwingine mjue hilo.”
WASOMAJI WETU
Baadhi ya wasomaji wa Magazeti Pendwa ya
Global Publishers wamekuwa wakipiga simu chumba cha habari na kuulizia
kama kesi ile ilifutwa kinyemela au kihalali.
“Jamani Global, mimi shida yangu ni
kuulizia kuhusu ile kesi ya Lulu na Kanumba. Hivi bado ipo au
ilishafutwa kinyemela. Maana si mnajua watu maarufu tena huenda kuna
kubebana,” aliwahi kuuliza msomaji mmoja.
LULU ASAKWA
Jumatatu
na Jumanne iliyopita, simu ya Lulu ilipopigwa iliita muda mrefu bila
kupokelewa. Hata hivyo, baadhi ya watu wake wa karibu walisema Lulu huwa
hapokei simu ambayo jina halipo kwenye simu yake.


Note: Only a member of this blog may post a comment.