Baada ya kuenea
kwa madai kuwa staa wa sinema za Kibongo, Kajala Masanja ‘Kay’
amepangishiwa bonge la mjengo na kigogo mmoja (jina kapuni), mumewe
Faraji Agustino anadaiwa kulizwa na vitendo vya mkewe huyo
vinavyomuumiza akiwa jela.
Mbali na kigogo huyo, pia mwanadada huyo
anadaiwa kutoka kimapenzi na msanii wa Bongo Fleva, Abbott Charles
‘Quick Rocka’, habari iliyoripotiwa na gazeti hili toleo lililopita
ambayo nayo wambeya walimfikishia na kumfanya ajisikie vibaya.
Habari kutoka kwa mmoja wa ndugu wa
Faraji ambaye amekuwa akimtembelea jela kumjulia hali zilidai kwamba,
Kajala amekuwa akimliza mwenza wake huyo kutokana na maneno ambayo
amekuwa akipelekewa kuhusu tabia zake za sasa huko mtaani.
“Kuna siku Kajala alikwenda kumtembelea
kule gerezani, Faraji akajisikia faraja sana na kuona kumbe mkewe bado
anampenda na kumjali. Siku chache baadaye akapata taarifa kuwa, mkewe
huyo anatoka na yule mwanamuziki sijui wanamuita Quick Rocka aliumia
sana na kujikuta akitokwa na machozi,” alisema mtoa habari huyo.
Baada ya kupata taarifa hizo, mwandishi
wetu alimtafuta Kajala na kumuuliza juu ya madai hayo, alipopatikana
alisema: “Kama mwezi mmoja hivi kabla ya kwenda mikoani kwenye hizi
harakati (kampeni) za CCM (Chama Cha Mapinduzi) nilikwenda kumuona na
kumjulia hali, yupo vizuri tu na wala hamna shida yoyote. Hayo ni maneno
ya watu tu.”
Machi mwaka jana, Faraji alihukumiwa
kifungo cha miaka saba jela au faini ya zaidi ya Sh. milioni 200 baada
ya kupatikana na hatia ya kutakatisha fedha haramu kwenye Benki ya NBC,
Tawi la Dar ambapo alishindwa kulipa kiasi hicho cha fedha na kujikuta
‘akiozea’ Gereza la Segerea hadi leo.
Katika msala huo uliomweka Faraji
gerezani, Kajala alihukumiwa miaka mitano kwenda jela na mumewe huyo
lakini mwanadada huyo alilipiwa faini ya Sh. milioni 13 na Wema Isaac
Sepetu.

Note: Only a member of this blog may post a comment.