Msimamo: Taifa hilo kubwa duniani limeshikilia msimamo wake kwamba bado
kuna rushwa kubwa hapa Tanzania na hivyo hakutakuwa na misaada ya kimaendeleo mpaka hapo hatua zitakapochukuliwa na serikali.
Taarifa iliyotolewa jana na MCC ilieleza kuwa mkutano wa robo ya mwaka wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo linalomilikiwa na serikali ya Marekani kwa ajili ya kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea ulijadili pendekezo la mkataba mpya na serikali ya Tanzania wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 472.8 na kuamua kuwa fedha hizo zitolewe baada ya Tanzania kutimiza kigezo cha kuzuia rushwa. Ilielezwa kuwa msaada huo ni maalum kwa ajili ya kuimarisha sekta ya umeme nchini, lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.
Kadhalika, ilieliezwa kuwa msaada huo ungehusisha pia uimarishaji wa taasisi zinazohusika na usambazaji wa umeme na usimamizi wake, kusaidia utekelezaji wa mipango ya mageuzi katika sekta ya nishati na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi.
Hata hivyo, taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya mkutano huo uliofanyika juzi (Septemba 17), Bodi ya Wakurugenzi wa MCC ilitoa taarifa rasmi ya kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya mageuzi muhimu kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wenye ufanisi wa mkataba, lakini haitapewa msaada huo hadi itakapofaulu kigezo cha kiashiria cha kuzuia rushwa (Control of Corruption indicator).
“Pamoja na kutambua mageuzi hayo, Bodi iliendelea kuelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania na kukubaliana kwamba ni lazima kwanza Tanzania ifaulu kufikia kigezo cha udhibiti wa Rushwa (Control of Corruption indicator) katika tathmini ya mwaka 2016 ya jinsi nchi husika zinavyokidhi vigezo vya kusaidiwa na MCC,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ilimkariri Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress, akisema kuwa wanafurahishwa na jitihada za serikali ya Tanzania kuinua ufanisi katika sekta ya nishati lakini bado kuna kazi ya kufanywa kwani tatizo la rushwa linaendelea kuathiri karibu kila nyanja.“Tunafurahishwa na jitihada za Tanzania katika miezi kadhaa iliyopita za kufanya mageuzi ya kimuundo na kitaasisi ili kuinua ufanisi, tija na uwazi katika sekta ya nishati.
Hata hivyo, kama ambavyo Bodi ya MCC imebainisha, pamoja na jitihada kadhaa zilizochukuliwa kukabiliana na rushwa, bado tatizo hili limeendelea kuwa kubwa likiathiri nyanja zote za maendeleo na ufanisi katika utendaji wa serikali.”
Taarifa inaeleza kuwa kwa kawaida, shughuli za MCC hufanyika katika msingi wa kuamini kuwa msaada unaotolewa unaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi ikiwa unaimarisha pia utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu kwa nia ya kukuza uchumi na kuondoa umasikini.
Kashfa ya Escrow
Katika taarifa yake, Bodi ya MCC haikutaja tukio lolote la rushwa linalowapa hofu katika kutekeleza mktaba huo mpya wa dola milioni 472.8. Hata hivyo, miongoni mwa matukio makubwa yaliyotikisa nchi hivi karibuni ni sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, ambalo lilisababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu na vigogo kadhaa kufikishwa mahakamani na wengine kupelekwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Mpaka sasa mhusika mkuu katika kashfa hiyo Harbinder Singh Sethi bado hajakamatwa na kufunguliwa mashtaka na vyombo husika kama ilivyoagizwa na Bunge mwishoni mwa mwaka jana.
Aidha baadhi ya vigogo toka CCM walihusika katika kashfa hii wamepitishwa na chama hicho mapema Julai kugombea nafasi kadhaa za uongozi ikiwamo ubunge, licha ya baadhi yao kulazimishwa kujiuzulu nyadhifa zao mapema mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE


Note: Only a member of this blog may post a comment.