Edward Lowassa.
Nassor Gallu, Dar es Salaam
ILE kambi ya Yanga SC, iliyotarajiwa kuwekwa Bagamoyo kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara kuanzia Jumamosi hii, imelazimika kuvunjwa chanzo kikiwa ni wagombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli na yule wa Chadema kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
ILE kambi ya Yanga SC, iliyotarajiwa kuwekwa Bagamoyo kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara kuanzia Jumamosi hii, imelazimika kuvunjwa chanzo kikiwa ni wagombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli na yule wa Chadema kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Yanga iliyo chini ya Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ilipanga kuanza
kambi hiyo leo na kujipanga zaidi kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza
dhidi ya Coastal Union ya Tanga, Jumapili hii lakini sasa mpango huo
‘umefukiwa’ na sasa timu hiyo itabaki jijini Dar mpaka ligi hiyo
itakapoanza.
Imeelezwa kuwa kila kitu kilikuwa kimepangwa sawia lakini ghafla
baada ya Lowassa kurejea Dar akitokea mikoani kwa ajili ya kuja kupiga
kampeni, uongozi wa Yanga ukabaini kuwa hilo linaweza kuondoa umakini wa
kujikita na maandalizi yao na badala yake wakahamia kwenye kufuatilia
siasa.
Hiyo imekuja baada ya kuvuja kwa ratiba inayoeleza kuwa Lowassa anaweza
akatua Bagamoyo hivi karibuni kwa ajili ya kwenda kunadi sera zake,
hivyo Yanga ikaamua kuuepuka mgongano huo ikiwemo pia kuingiliana katika
suala la utumiaji wa viwanja.
Championi Jumatano limezungumza na Mkuu wa Kitengo cha Habari na
Mawasiliano cha Yanga, Jerry Muro na kubainisha kwamba wamebadili upepo
ghafla kutokana na wimbi la kisiasa ambalo sasa limehamia katika ukanda
huo, huku viwanja na sehemu nyingi za wazi zikitumiwa zaidi na wanasiasa
katika kunadi sera zao ili kuwashawishi wananchi wawapigie kura katika
Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
“Kambi ya Bagamoyo tumeivunja, tumeamua kubaki hapahapa Dar kwa ajili ya maandalizi ya siku chache kabla ya ligi kuanza. Kweli tulipanga kwenda Bagamoyo kesho (leo), lakini tukatafakari hizi ishu za siasa tukaona zitatupotezea utulivu na pia viwanja vingi vinatumika wakati huu, hivyo tunaweza kupata changamoto.
“Lakini kingine ni kwamba tuliamua tukae Bagamoyo kisha tufanye mazoezi
Dar pale kwenye Uwanja wa Boko, bado tukaona ni kujitesa na kuwachosha
wachezaji. Kwa kuliangalia hilo, tumeamua kuendelea na programu zetu
tukiwa Dar.
“Tutaendelea kujifua palepale kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi kwa
ajili ya sababu za kiufundi tayari kwa kampeni ya kutetea ubingwa na
kushiriki vyema michuano ya kimataifa. Kama unavyojua sisi ni wa
kimataifa,” alifafanua Muro aliyetoswa kwenye kura za maoni za kuwania
ubunge katika Jimbo la Kawe, Dar kupitia CCM.

Note: Only a member of this blog may post a comment.