Stori: Richard Bukos aliyekuwa Kagera
UNAZI! Kundi kubwa la vijana wa
kike na kiume, mwanzoni mwa wiki iliyopita walizua kizaazaa baada ya
kumgombea kumuona kwa karibu na kutaka kuzungumza na mkali wa muziki wa
Kizazi Kipya, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ mara baada ya kumaliza
kutumbuiza katika mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli uliofanyika katika Viwanja vya
Gymkhana mjini Bukoba.
Baada ya kumaliza ngwe yake ya
kuburudisha, msanii huyo aliteremka jukwaani na kwenda alikopangiwa
kukaa, lakini alifuatwa na dada mmoja aliyetaka kuzungumza naye, huku
vijana wengine wakisogea eneo hilo, kitu ambacho mabaunsa walikikataa na
kumfanya msanii huyo kukimbilia katika basi dogo aina ya Coaster
lililokuwa limetayarishwa kwa ajili yake na wacheza shoo wake.
Hata hivyo, wakati mkutano huo
ukiendelea, umati zaidi wa vijana uliendelea kulifuata basi hilo na
kujazana katika dirisha alilokaa Diamond, jambo lililowapa wakati mgumu
mabaunsa kuwasogeza, hadi polisi walipofika na kufanikiwa kuwatawanya,
huku gari hilo likiondolewa eneo hilo.
Hata hivyo, baada ya basi hilo kupata
upenyo wa kumkimbiza mwanamuziki huyo, kundi kubwa la vijana wa kike na
kiume walilifukuza gari hilo mpaka dereva alipoongeza kasi.
Kabla ya mkutano huo mkoani hapa,
Magufuli alianza kunadi sera zake katika Vijiji vya Kaziramuyagwa,
Kyamyorwa, Kasharunga, Rulanda na kufanya mkutano mkubwa katika Uwanja
wa Zimbihile uliopo Muleba Kusini jimbo analogombea Prof. Anna
Tibaijuka.
Baada ya hapo kampeni zilihamia Muleba
Kaskazini ambapo Magufuli alimwaga sera katika maeneo ya viwanja vya
wazi vya Kamachumu, Maruku na Jimbo la Bukoba vijijini kabla ya kufanya
mkutano wa kihistoria katika viwanja vya Bukoba mjini.

Note: Only a member of this blog may post a comment.