Beki wa kati wa kimataifa raia wa Togo, Vincent Bossou.
Wilbert Molandi,Dar es SalaamSIKU moja baada ya kumpokea kiungo mkabaji Mzimbabwe, Yanga, jana asubuhi ilimpokea beki wa kati wa kimataifa raia wa Togo, Vincent Bossou aliyetua kwa ajili ya kuichezea timu hiyo msimu ujao wa 2015/2016.
Beki huyo mwenye uwezo wa kucheza namba zote za ulinzi wa kati, ametua kuichezea timu hiyo baada ya Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm kutoa mapendekezo ya kumsajili beki mmoja wa kati na habari njema ni kuwa amefuzu katika vipimo vya afya.
Bossou alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam muda wa saa 3:15 asubuhi tayari kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Yanga.Beki huyo, pamoja na Thabani Kamusoko, wote kwa pamoja walifuzu majaribio mafupi na vipimo vya afya kabla ya kupewa mikataba.
Akizungumzia juu ya vipimo hivyo, Daktari wa Yanga, Juma Sufiani alisema: “Bossou na Kamusoko wote wamefanyiwa vipimo leo (jana) na wapo vizuri, bahati nzuri wamefuzu katika vipimo hivyo vilivyofanyika kwenye Hospitali ya Agha Khan, kuna baadhi ya vipimo majibu yake yatatolewa kesho (leo), nadhani baada ya hapo watakuwa na jukumu la kumalizana na uongozi wa klabu.”
Bossou alitakiwa kufanya mazoezi na Yanga chini ya Pluijm na msaidizi wake, Charles Mkwasa lakini ilishindikana kutokana na kuchelewa kufika huku Kamusoko akifanikiwa kufanya baada ya kutua juzi Jumanne.
Beki huyo, kama akifanikiwa kufuzu vipimo vyote vya afya, basi atasaini kuichezea Yanga kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba kwenye timu ya Goyang Hi FC ya Korea Kusini.

Note: Only a member of this blog may post a comment.