WAKATI mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kuwapata wagombea wa nafasi ya udiwani na ubunge kwa tiketi ya chama cha mapinduzi ukiendelea kulalamikiwa katika maeneo mbali mbali nchini wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wagombea wanne wa nafasi ya ubunge wamejitokeza na kulalamikia mchakato huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Songea mkoani Ruvuma baada ya mchakato huo kukamilika na matokeo kutokutangazwa hadharani zaidi ya kujulishwa kwa simu kuwa mgombea Vita Kawawa ndiye aliyeshinda kitendo walichodai ni kinyume na taratibu na kanuni za uchaguzi ndani ya chama.
Wagombea hao wamewalalamikia baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi ya wilaya kwa kujijuhusisha na kampeni za wazi za kumnadi mgombea mmoja ambaye ni chaguo lao mchakato walioanza kuufanya mapema kabla ya mchakato rasmi ndani ya chama kwa wagombea wote kujinadi kuanza kitendo ambacho ni kinyume na taratibu za uchaguzi wa ndani ya chama.
Wamewataja viongozi waliohusika na vitendo hivyo kuwa ni mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Namtumbo Benjamin Nindi,katibu wa chama cha mapinduzi wilaya ya Namtumbo Mohamed Aziz na katibu mwenezi wa chama cha mapinduzi wilayani Namtumbo Kasimu Gunda.
Wamesema ukiukwaji huo wa taratibu ulioanza mapema kabla ya muda wa kuanza kwa kampeni za kujinadi kwa wagombea uliwafanya baadhi ya wagombea kumkataa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilayani humo kusimamia kampeni hizo kwa kitendo cha kuonesha kumbeba mgombea mmoja kati yao na taratibu za kumuondoa kusimamia zilifanyika.
Wagombea hao wanne ambao ni Salum Homera(467),Charles Fussi(1122),Ally Mbawala(1783) na Alufrio Nchimbi(817) wamepinga kitendo cha kutaka kurudiwa kwa zoezi hiklo la uchaguzi wa kura za maoni kwa nafasi ya ubunge ambalo limepangwa kufanyika kesho kwa maelekezi yaliyotolewa kwao na katibu wa chama cha mapinduzi mkoa wa Ruvuma Verena Shumbusho kwa madai kuwa muda huo ni mfupi na wapiga kura wameshasambaa huku wengine wakiwa wameshaenda mashambani.
Pamoja na kuwa wanaowalalamikia ni wagombea wenzao wawili ambao ni Vita Kawawa aliyeibuka mshindi kwa kupata kura 9,287 pamoja na Edwin Ngonyani aliyepata kura 7,856 wamesema ni vyema matokeo hayo yakaheshimika na kama suala ni kurudia uchaguzi uchaguzi muda uliowekwa hautoshi kwa zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa wapiga kura na wagombea.
Wagombea wengine ambao hawajasema chochote kuhusiana na mchakato huo pamoja na kura walizopata ni Vintan Kilowoko(3118),Julius Luena(1058)Salome Sijaona(7195),Musa Chowo(2764) na Edwin Milinga(1794).

Note: Only a member of this blog may post a comment.