Jioni moja
nikiwa nimekaa chini ya mti na babu yangu, Mzee Kahungo tukipunga upepo
na kubadilishana mawazo, nilipoenda kumtembelea kijijini Magoma, Korogwe
mkoani Tanga hivi miezi kadhaa iliyopita, alikuja mwanaume wa makamo
akiwa na uso uliosawijika, macho yakiwa yamebadilika rangi na kuwa
mekundu.
Alikuwa akihitaji ushauri kutoka kwa babu yangu, nilitaka kuinuka na kuwapisha kama zilivyo mila na tamaduni za kwetu kuwapisha wakubwa wanapozungumza mambo yao lakini babu alinitaka nami nisikilize kile alichotaka kukieleza mgeni huyo, nikaketi vizuri na kuanza kusikiliza kwa umakini. Mwanaume huyo alimwambia babu kwamba ameishi na mkewe kwa miaka 26 na kufanikiwa kuzaa watoto watano lakini baadaye amegundua kwamba mwanamke huyo hamfai, ana tabia mbaya, hana mapenzi ya kweli na kuhitimisha kwamba alikuwa ameamua kumpa talaka.
Nilimuona babu akitabasamu, akavuta moshi mwingi wa tumbaku kwenye kiko kisha akaupuliza hewani na kumgeukia yule mgeni, akamwambia kwamba kama ameweza kuishi na mwanamke kwa muda wa miaka 26 bila kugundua kasoro zake mpaka muda huo kama mwenyewe alivyosema, basi mwenye matatizo siyo mke bali ni yeye mwenyewe.
Akaendelea kumwambia kwamba kwa kawaida kasoro za namna hiyo, huonekana mapema kabisa baada ya kuingia kwenye ndoa na ni jukumu la muoaji kuchukua hatua mapema lakini si baada ya miaka 26, akasisitiza kumwambia kwamba yeye ndiye mwenye matatizo kwa sababu alishindwa kubaini upungufu wa mkewe kwa kipindi chote cha miaka 26 waliyoishi pamoja.
Mazungumzo yaliendelea kwa muda mrefu lakini mwisho, yule mwanaume aliamua kubatilisha uamuzi wake wa kumuacha mkewe huyo na kuahidi kwamba anakwenda kuzungumza naye kwa kina ili kumaliza tatizo lililokuwa likiisumbua ndoa yake.
Nilishindwa kuificha furaha niliyokuwa nayo, waliosema mtu mzima dawa hawakukosea, babu yangu alikuwa dawa haswaa!
Lengo la kuanza na mfano huo hapo juu ni kuhusu vuguvugu la wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukihama chama hicho na kukimbilia upinzani linalozidi kushika kasi kila kukicha.
Makada waliokulia ndani ya CCM, wengine wakiwa wamekitumikia kwa miaka kibao, leo wanasimama hadharani na kukitukana chama. Wanausema udhaifu wake wakiwa wameshasahau kwamba wamekaa miongo kadhaa ndani ya chama hicho! Wanamtukana mke au mume ambaye wameshaishi naye miaka kibao na kuzaa naye watoto!
Ni mwendawazimu pekee anayeweza kuziamini sababu wanazozitoa. Kwa mwenye akili timamu lazima atakuwa ameshagundua ni jambo gani lililojificha nyuma ya wimbi hilo la makada wanaokihama CCM na kukimbilia upinzani.
Wa kwanza kutangaza uamuzi wa kukihama CCM, chama ambacho ndicho kilichomlea na kumkuza kisiasa kwa miaka yote, alikuwa ni waziri mkuu aliyejiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond, Edward Ngoyai Lowassa.
Lowassa alitangaza kujivua uanachama wa CCM na kuhamia Chadema, zikiwa ni siku chache baada ya jina lake kukatwa kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Ipo wazi kwamba Lowassa alikatwa kwenye hatua za awali za mchakato huo kutokana na rekodi yake ya maadili kwani amekuwa akituhumiwa mara kwa mara kuhusika na kashfa zilizoigharimu serikali mamilioni ya fedha.
Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa chama hicho ambacho siku zote husimamia usafi wa kimaadili wa viongozi au wanasiasa wanaowania uongozi kwa tiketi yake, Lowassa aliamua kuhamia Chadema huku akitoa maneno mengi yasiyo ya kiungwana, akiituhumu CCM kwa mambo chungu nzima, akiwa amesahau kabisa kwamba chama hicho ndicho kilichomkuza mpaka hapo alipofikia.
Tangu Lowassa alipojiunga Chadema, wagombea wengine wa nafasi mbalimbali, kuanzia udiwani hadi ubunge kutoka CCM wameendelea kuhamia Chadema. Ukijaribu kufuatilia kwa kina, kila anayeihama CCM na kukimbilia Chadema, anayo sababu binafsi iliyomfanya kuchukua uamuzi huo.
Makongoro Mahanga, Mbunge wa Segerea anayemaliza muda wake ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, naye ni miongoni mwa walioihama CCM na kukimbilia Chadema.
Japokuwa mwenyewe haelezi moja kwa moja kilichosababisha akachukua uamuzi huo, ipo wazi kwamba aliamua kuhamia Chadema baada ya kuanguka kwenye kura za maoni za kutetea nafasi yake ya ubunge wa Segerea.
Kama ilivyokuwa kwa Lowassa, Mahanga naye alitoa sababu nyepesi za kukihama chama hicho, huku akiwa mzito kueleza ukweli kwamba amehama kwa masilahi yake binafsi kwa sababu ameangushwa kwenye kura za maoni. Matokeo yake naye akawa kama yule mwanaume aliyekuja kuomba ushauri kwa babu yangu!
Orodha inazidi kuongezeka na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo wafuasi wengine wa CCM ambao wameonekana si lolote ndani ya chama hicho (makapi), iwe ni kwa wao wenyewe kukosa maadili ndani ya chama, kukatwa kwenye vinyang’anyiro vya kura za maoni au ndugu zao wa karibu kukatwa, wameendelea kuhamia Chadema.
Kwa hiyo ukipima kwa kina utagundua kwamba wote wanaoihama CCM ni kwa sababu wametanguliza masilahi yao binafsi badala ya masilahi ya chama na wananchi wa Tanzania, kila mtu anatetea tumbo lake. Hakuna kiongozi hata mmoja kutoka CCM mwenye maadili ambaye ametangaza kukihama chama hicho.
Wanaofanya hivyo ni wale makapi ambao wamegundua kwamba mfumo wa CCM unawakataa kwa sababu ya kuendekeza vitendo vinavyowachukiza binadamu wenzao na Mungu wao. Watanzania wawe makini na matapeli hawa wa kisiasa wanaotanguliza matumbo yao mbele.
Huwezi kukwepa ngumi ya uso kwa kufumba macho!
Note: Only a member of this blog may post a comment.