KWENU
Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), bila shaka mko poa na mnaendelea na
kazi zenu za kila siku. Nimewakumbuka leo kupitia barua nzito.
Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima wa afya. Namshukuru Mungu kwa kunipa uzima na kunuwezesha nguvu ya kuweza kuwaandikia barua hii. Kwanza nianze kwa kuwapongeza kwa kile mlichokifanya. Kumsimamisha msanii Zuwena Mohamned ‘Shilole’ kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na tukio lake la kucheza jukwaani akiwa nusu utupu.
Japo yawezekana ilikuwa bahati mbaya nguo ile kumtoka akiwa jukwaani lakini kwa kuwa mlimuita na kumtaka ajieleeze, akakaidi, hata mimi naungana nanyi Basata.
Mlistahili kutoa adhabu kubwa ili iwe fundisho si tu kwa sababu ya tukio lake la kucheza nusu utupu lakini pia kutokana na ukaidi aliounesha wa kukataa kujieleza kwa nini asiadhibiwe.
Kuheshimu mamlaka inayosimamia jambo fulani siku zote ni suala la msingi. Sitaki kuamini kama usingewapuuza Basata wangekuadhibu adhabu kubwa kiasi hicho.
Ungeenda kuzungumza nao mimi naamini kabisa pengine wangekupa adhabu ndogo kama si kukuonya tu!
Ulipopuuza umewaongezea hasira bila wewe kujua. Ungeenda na kuwaelezea mazingira ya tukio, au ungewaandikia barua kuwaelezea mazingira ya tukio, lingekuwa jambo la busara na pengine isingetoka adhabu hiyo, najua inauma lakini sina jinsi zaidi ya kukuambia pole.
Nikirudi kwenu ndugu zangu wa Basata, kwanza nataka niwaambie tu, pamoja na kuona tatizo hilo la Shilole, yapo mengi sana ambayo yanatokea kwenye sanaa yetu lakini bado mmekuwa mkiyafumbia macho.
Zipo video nyingi tu za wasanii wetu ambazo ukizitazama hazifanani na maadili ya Mtanzania lakini tunashuhudia zikichezwa katika vituo mbalimbali vya Runinga nchini.
Ukiachana na video hizo, zipo sinema ambazo zimechezwa na wasanii wetu ambazo pia ukiziangalia kwa makini huwezi kusema zinaendana na maadili ya Mtanzania. Kwa nini mmekaa kimya eneo hilo? Wachukulieni hatua ili kusiwe na malalamiko.
Mliwahi pia kuzuia ngoma zile zinazokesha mitaani, zikihusisha wadada wanaocheza utupu kabisa, ndani ya muda mfupi tuliona zimerudi tena na zinapigwa kama kawa.
Kwa kuwa mmeonesha kushughulikia sanaa yetu basi hakikisheni kweli kazi zote za sanaa mnazikagua vema kabla ya kuwafikia Watanzania.
Makucha yenu kweli yaonekane, kuna nyimbo nyingi tu zinapigwa redioni zikiwa na lugha ya matusi, zishughulikieni ili kulinda maadili ya Watanzania.
Kwa leo ni hayo tu,
Wasalaam Erick Evarist

Note: Only a member of this blog may post a comment.