MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imepanga kutoa hukumu ya rufaa iliyokatwa na Mawaziri wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona,
Septemba 18, mwaka huu baada ya kupitia hoja za upande wa utetezi na mashtaka.
Tarehe hiyo ya kutolewa uamuzi rufaa hiyo ya kupinga adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kilichotolewa kwa mawaziri hao wa zamani ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Projest Rugazia.
Mahakama iliridhia jana Mbele ya Jaji Rugazia kuwa Agosti 12 mwaka huu pande zote mbili zitawasilisha hoja za kesi hiyo kwa maandishi Agosti 12 na Agosti 19 pande zote mbili zitajibu hoja zilizowasilishwa na Agosti 26 itakuwa kwa ajili ya majumuisho.
Katika rufaa hiyo upande wa utetezi unawakilisha na jopo la mawakili watano wakiongozwa na Richard Rweyongeza.
Upande huo wa utetezi ulieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilifikishwa kwa ajili ya kusikilizwa na kuunganishwa, hivyo wako tayari kuendelea baada ya kupitia taarifa zao.
Rweyongeza alidai kwamba wamekubalina pande zote mbili kesi hiyo isikilizwe kwa maandishi.
Alidai sababu za kukataa rufaa ni kutokana na hati ya mashtaka iliyowatia wateja wake hatiani kuwa na mapungufu ya kisheria na kwamba mahakama ya chini ilikosea kwa kutowaamini Yona na Mramba kulipa zile fedha.
Alitaja sababu ya tatu wa mahakama ilikosea kisheria kwa kuwatia hatiani kinyume na msingi ambayo imekwishawekwa katika makosa ya jinai ambayo hitaji la kuthibitisha nia ya Mramba na Yona kama kigezo muhimu katika shtaka la kwanza hadi la 10 la matumizi mabaya ya madaraka.
Rweyongeza alidai sababu ya nne mahakama ilikosea kisheria kwa kuwatia hatiani wakati hakukuwepo na ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa mbele yao, tano adhabu iliyotolewa dhidi yao haikustahili na ilikuwa kubwa.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 6, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya jopo la mahakimu watatu ambao ni Hakimu Saul Kinemela, Jaji Sam Rumanyika na Jaji John Utamwa baada ya kukutwa na hatia ya mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7.

Note: Only a member of this blog may post a comment.