Thursday, August 20, 2015

Anonymous

HABARI MBAYA Kwa Mashabiki Wanazi wa YANGA SC

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limemtangaza refa, Israel Nkongo wa jijini Dar es Salaam kuwa ndiye atakayechezesha mechi ya Ngao ya Jamii itakayowakutanisha mabingwa wa msimu uliopita, Yanga dhidi ya Azam, Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.

Nkongo ndiye mwamuzi ambaye Yanga wamekosa bahati naye kwani ndiye aliyechezesha mechi waliyopigwa 5-0 dhidi ya Simba Mei 6, 2012 na pia waliyolala 3-1 dhidi ya Azam Machi 11, mwaka huohuo, ambayo wachezaji wa mabingwa hao walimpiga na kukumbana na adhabu za vifungo.
Katika mechi hiyo dhidi ya Azam pia, kiungo Haruna Niyonzima na nahodha Nadir Haroub 'Cannavaro' walitolewa kwa kadi nyekundu, huku Stephano Mwasyika akikumbana na adhabu ya kufungiwa mwaka mzima kwa kumpiga ngumi Nkongo uwanjani wakati wa vurugu za wachezaji wa Yanga dhidi ya mwamuzi huyo.  
Nkongo na wasaidizi wake walitoka siku hiyo kwa kusindikizwa na askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) baada ya kupuliza kipenga cha mwisho kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. 
Katika mechi ya keshokutwa, Nkongo atasaidiwa na Samuel Mpenzu kutoka jijini Arusha, Josephat Daud Bulali (Tanga) na mwamuzi wa akiba atakuwa ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamisaa wa mchezo huo atakuwa Deogratius Rwechungura kutoka mkoani Mara.
Akizungumza jana jijini, Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Baraka Kizuguto, alisema kuwa mechi hiyo itaanza saa 10:00 jioni na endapo hatapatikana mshindi ndani ya dakika 90, hatua ya penalti itafuata.
Kizuguto alitaja kiingilio cha chini katika mchezo huo kuwa ni Sh.7,000 kwa eneo la viti vya rangi ya kijani, bluu na rangi ya machungwa wakati VIP B na C mashabiki watalipia Sh.20,000.
Alisema kuwa tiketi zitauzwa siku ya mchezo na mashabiki watakata tiketi za VIP A watalipia Sh 30,000 kila mmoja. 
CHANZO: NIPASHE

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.