Friday, August 21, 2015

Anonymous

DAR Marufuku Kushikana Mikono!

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amepiga marufuku uuzwaji wa vyakula na matunda katika maeneo yasiyo rasmi pamoja na kushikana mikono. 

Agizo hilo limelenga kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea kusambaa katika jiji la Dar es Salaam, ambapo hadi sasa watu watatu wameripotiwa kupoteza maisha. 

Sadick alitoa amri hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema wagonjwa wa kipindupindu wamefikia 56.
“Wagonjwa wameendelea kupokelewa na hadi jana walikuwa wamefikia 56 wakitokea maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama, Kimara, Saranga, Manzese, Kigogo, Tandale na Mwananyamala, maeneo yote yakiwa Manispaa ya Kinondoni.
“Wagonjwa 36 kati yao wamelazwa katika kambi maalum tulizotenga,17 wametibiwa na kuruhusiwa na watatu wamefariki hadi sasa,” alisema. 

Alisema kutokana na hali hiyo ni lazima jamii na serikali kwa ujumla ikachukua hadhari vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya.
Alisema, ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, serikali mkoani humo imepiga marufuku uuzwaji wa vyakula mitaani pamoja na mikusanyiko katika misiba ya watu wanaopoteza maisha kwa ugonjwa huo. 

Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyokaribu nao iwapo watagundua mtu mwenye dalili za ugonjwa huo. 

Alitaja dalili zake kuwa ni pamoja na kutapika, kuharisha mfululizo choo cha majimaji meupe, ngozi kusinyaa, kiu kali, midomo kukauka, mapigo ya moyo kwenda mbio, kuumwa na misuli na mwili kukosa nguvu.
“Imefika wakati wananchi wanatakiwa kubadilika na kujua kwamba, suala la usafi ni la kila mtu.
“Tusisubiri  serikali ije itufayie tuone kuwa uchafu ni adui yetu, tuwe wa kwanza kusafisha mazingira yetu ili tuwe salama,” alisema. 

Wakati Sadiki akieleza hayo, uchafu kwenye maeneo mbalimbali ya jiji umekithiri, huku pia vyakula vikipikwa na kuuzwa kwenye maeneo yasiyo salama. 

Kwenye eneo la Buguruni Maruzuku Kata ya Mnyamani Wilaya ya Ilala, hali ya mazingira si nzuri kutokana na mitaro kujaa uchafu na kusababisha  maji taka kutuwama. 

Fatuma Nasoro ambaye ni mfanyabiashara wa chakula na mjumbe wa nyumba 10 kwenye eneo hilo, alisema magari makubwa yamekuwa yakichangia kuharibu mitaro hali ambayo inachangia kutuwama kwa maji taka katika maeneo ya nyumba zao ambazo zimezungukwa na mitaro hiyo.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.