Sweetbert Lukonge,Dar es Salaam
USAJILI uliofanywa na Simba mpaka sasa umeonekana kuwa gumzo na inavyoonekana timu hiyo inaweza kufanya vizuri katika msimu ujao kama itaendelea na moto ambao inauonyesha katika mechi za maandalizi.
Akizungumza na Championi Ijumaa, nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alikuwa mmoja wa watu wa timu hiyo ya Jangwani kukiri kuwa Simba wanaweza kuwasumbua msimu ujao unaotarajiwa kuanza Septemba 12, mwaka huu.
“Simba ya safari hii itakuwa ni tofauti kabisa na ile ya msimu uliopita, nimekuwa nikifuatilia usajili wao, inavyoonekana imesajili watu wa kazi, hivyo kazi ipo msimu ujao, inabidi tujipange vilivyo ili tuweze kutetea ubingwa wetu,” alisema Cannavaro na kuongeza:
“Simba ndiyo wapinzani wetu wakubwa, ndiyo maana kuwafuatilia siyo jambo baya, siyo mimi peke yangu, wengi tunawafuatilia wao, huwezi kusema Azam ni wapinzani wetu wakubwa, hapana, Simba ndiyo wapinzani zaidi kwetu.”
Simba haikufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara kwa misimu mitatu iliyopita, kwa sasa inaonekana kufanya usajili wa nguvu ikiwa ni moja ya mbinu za kurejesha ufalme wake uliopotea kwa miaka kadhaa ambapo imeshinda mechi zote sita ilizocheza kujiandaa na msimu mpya.
Baadhi ya wachezaji wapya wa Simba ni Mwinyi Kazimoto, Mussa Mgosi, Justice Majabvi (Zimbabwe), Hamis Kiiza (Uganda), Emily Namubona (Burundi) na Vincent Agban (Ivory Coast).
Note: Only a member of this blog may post a comment.