Wiki iliyopita
niliishia pale ambapo Al-Shabaab walipoanzisha mapambano dhidi ya
majeshi ya serikali huku wakihusishwa na mauaji ya watu 70 katika Jiji
la Kampala nchini Uganda.
SASA ENDELEA…
Baada ya mapigano kuwa makali kati ya serikali ya Somalia huku wakisaidiwa na nchi jirani ikiwemo Ethiopia na Kenya, Al-Shabaab waliamua kuweka vikwazo vya kuingizwa bidhaa hasa vyakula kutoka kwenye sehemu za Mkoa wa Bay nchini humo, wakazi na maafisa wa huko walieleza wasiwasi wao juu ya kuzorota kwa hali ya kibinadamu hasa baada ya kuwepo kwa tishio la njaa kali ambapo wazee na watoto walipoteza maisha kwa idadi ambayo haikujulikana mara moja. Ilibidi maafisa wa Misheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia katika Mji wa Baidoa, Mji Mkuu wa Mkoa wa Bay kuingilia kati na kutoa huduma za kiafya na chakula.
Kizuizi hicho cha Al-Shabaab kilianza Oktoba 19, 2012. Kizuizi hicho kiliathiri vijiji vingi vilivyokumbwa na baa la njaa kwenye viunga vya Bardale ambao ni mji mwingine mkoani Bay, Somalia.
Al-Shabaab walizuia magari kusafirisha chakula na bidhaa muhimu kupita kwenye maeneo yaliyoathirika pia walizuia magari ya mizigo yaliyokuwa yakisafirisha nafaka na malighafi za viwandani.
Kwa mujibu wa Meya wa Bardale, Mohammad Isaq Hassan, Al-Shabaab walisababisha ugumu wa maisha uliotishia usalama wa chakula kwa jamii zilizoathirika.
Al-Shabaab waliweka vizuizi vya barabarani kati ya maeneo yaliyoathirika, wakizuia kupelekwa vyakula muhimu kutoka mji mkuu wa mkoa huo, Baidoa.
Bulo Hawo, Tosh Weyn na Kurtun ni kati ya vijiji vilivyowekewa vizuizi na Al-Shabaab, matokeo yake ni kwamba wakazi wa huko walikabiliwa na hali mbaya ya maisha.
Bei ya chakula ilipanda maradufu. Gunia la sukari lilifika hadi dola 80 (zaidi ya shilingi 170,000) kutoka bei ya awali ambayo ilikuwa nusu yake, yaani dola 40. Vyakula vingine pia vilipanda sana bei.
Katika Kijiji cha Kurtun, mkazi wake, Ali Omar (35) ambaye alikuwa na mke na watoto watatu, alisema hawezi tena kununua chakula kwa ajili ya familia yake kwa sababu ya kupanda sana kwa bei ya vyakula kutokana na kizuizi hicho.
Ilibidi serikali ya shirikisho ya Somalia na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM) kuchukua hatua za haraka kuvunja kizuizi hicho.
Hata hivyo, kutokana na hali ya wanajeshi kupungua sana, operesheni hizo zilipunguzwa kwa sababu AMISOM ilikuwa ina jukumu lingine la kulinda miji au maeneo ambayo yalikwishabomolewa na Al-Shabaab.
Kizuizi hicho kilikuwa na athari nyingine ya kuwalazimisha madereva wasifanye kazi yao hiyo iliyokuwa ikiwaingizia kipato.
Al-Shabaab walikuwa wakiwaamuru kugeuza malori yaliyobeba chakula cha msaada na wakiwaambia chakula hicho kipelekwe kwa makafiri.
Kizuizi hicho kiliwalenga watu walioishi kwenye maeneo ya Mkoa wa Bay ambayo yalikuwa kwenye mikono ya Al-Shabaab kabla ya kuingia kwenye mikono ya majeshi ya serikali na washirika wake.
Baada ya wiki mbili, majeshi hayo yalifanikiwa kuzima kizuizi hicho lakini tayari vifo vilikuwa vimetokea vilivyosababishwa na njaa. Kilichofuata ni mfululizo wa mashambulio ya Al-Shabaab hasa kwa nchi ya Kenya.
Usikose wiki ijayo.
Note: Only a member of this blog may post a comment.