Sifael Paul
Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumesikika mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu wengi yanayofanywa na kundi haramu la kigaidi linaloitwa Al-Shabaab. Swali ni je, hawa Al-Shabaab ni nani hasa? Ungana nami katika simulizi ya Al-Shabaab itakayokujia kila Jumamosi kwenye safu hii. Jina Al-Shabab linamaanisha KIJANA kwa Lugha ya Kiarabu. Ni kundi lililoibuka miaka ya 2000 kama tawi la vijana la muungano wa Mahakama za Kiislam nchini Somalia barani Afrika likiwa na nguvu katika eneo la pwani ya nchi hiyo.
Baadaye mwaka 2006, muungano huo ulivunjika wakati kundi hilo lilipopigana na wanajeshi wa Ethiopia waliokuwa wameingia nchini Somalia kuunga mkono serikali iliyokuwa dhaifu.
Al-Shabaab hawakupendezwa na huwa hawataki majeshi ya nchi nyingine kuingilia Somalia. Wapo tayari kufanya matukio makubwa ya kigaidi katika nchi yoyote inayojifanya kusaidia serikali ya Somalia katika kupambana nao.
Kuna taarifa chungu nzima kuhusu wapiganaji wa Kiislam wanaokwenda Somalia kupigania Al-Shabaab.
Kundi hilo limeweka sheria kali za Kiislam katika maeneo ambayo linayadhibiti ikiwemo kupigwa kwa mawe hadi kufa wanawake wanaodaiwa kufanya uasherati pamoja na kuwakata wezi mikono.
Je, Al-Shabaab linadhibiti sehemu gani ya Somalia? Ingawa kundi hilo limepoteza udhibiti wa miji mikubwa kwa sasa, bado linakita mizizi katika maeneo yenye mashina yake kwenye miji tofauti nchini Somalia.
Lililazimika kuondoka katika Mji Mkuu wa Somalia, Mogadishu, mwezi Agosti mwaka 2011, kufuatia mashabulizi ya majeshi serikali ya Somalia kwa msaada wa jamii ya kimataifa. Pia lililazimika kuondoka katika mji wa bandarini wa Kismayo, mwezi Septemba mwaka 2012.
Kismayo ulikuwa mji muhimu kwa kundi hilo kwani ulikuwa unawezesha bidhaa kuwafikia wapiganaji wa kundi hilo pamoja na kuwatoza watu ushuru kwa shughuli zilizoendelea bandarini hapo. Baadaye walidaiwa kujihusisha na utekaji wa meli kubwa za mizigo na silaha kisha kupora mali katika Bahari ya Hindi.
Muungano wa Afrika (AU) ambao unaunga mkono juhudi za majeshi ya serikali ya Somalia, ulisherehekea ushindi huo ingawa Al-Shabaab hufanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kujitoa mhanga mjini Mogadishu na kwingineko.
Wadadisi wanaamini kuwa Kundi la Al-Shabaab lilianza kufanya mashambulizi ya kuvizia baada ya kushindwa na majeshi ya AU (African Union) wanaotumia nguvu dhidi yao.
Kundi hilo linakabiliwa na tishio kubwa kutoka kwa wanajeshi wa Kenya ambao walianza harakati zao dhidi ya kundi hilo kuanzia mwaka 2011.
Pamoja na ukorofi wa kundi hilo linalomiliki silaha kali za kivita na kijadi, Kenya ilituhumu wapiganaji wa Al-Shabaab kwa kuwateka nyara wanajeshi wake pamoja na watalii na sasa wamekuwa katika msitari wa mbele kupambana nao. Kenya imepakana na Somalia kwa upande wa Kusini.
Kwa upande wao, wanajeshi wa Ethiopia waliweza kukabiliana na wapiganaji hao na kudhibiti miji yao ya Beledweyne na Baidoa. Ethiopia imepakana na Somalia kwa upande wa Magharibi.
Baadaye kuliibuka taarifa za mgawanyiko katika kundi hilo ambazo hata hivyo, zinapingwa vikali na kundi lenyewe. Inaarifiwa kuwa uongozi wake unapingwa na wanachama wanaotoka maeneo ya Kusini mwa Somalia na ambao ni wengi katika kundi hilo. Inakisiwa idadi yao ni kati ya wanajeshi 7,000 hadi 9,000.
Kuna taarifa kuwa baada ya kuwa tishio na kuvuka mipaka ya Somalia wakishambulia maeneo tofauti duniani, Al-Shabaab walijiunga na lile kundi lingine la kigaidi la hatari duniani la Al-Qaeda, mwezi Februari mwaka 2012.
Katika kipindi hicho mmoja wa viongozi wa Al-Shabaab, Ahmed Abdi Godane alikaririwa akiahidi kumuunga mkono mmoja wa viongozi wa Al-Qaeda, Ayman Al-Zawahiri.
Kolabo ya makundi hayo mawili imekuwa tishio ikidaiwa kuungwa mkono na raia wa kigeni ambao wamekuwa wakisaidia harakati zao za mapigano kwa kuwafadhili kifedha ili kufanya biashara ya silaha.
Mwaka jana maafisa wa Al-Shabaab waliambatana na mtu aliyesema ni mwanachama wa Al-Qaeda na kumtambua kuwa raia wa Marekani, Abu Abdulla Almuhajir alipokuwa anatoa msaada wa chakula kwa waathiriwa wa njaa nchini Somalia.
Maafisa nchini Marekani wanaamini kuwa wapiganaji wa Al-Qaeeda ambao hawajahusiana sana na mashambulizi nchini Afghanistan na Pakistan kufuatia mauaji ya kiongozi wao, Osama bin Laden, wapiganaji wake wengi wanakwenda kutafuta hifadhi nchini Somalia.
Itaendelea wiki ijayo.

Note: Only a member of this blog may post a comment.