Mambo yamekuwa mazito. Ndivyo
inavyoonekana baada ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) kushindwa kutangaza mgombea urais jana badala yake
ukatoa ahadi mpya kwamba sasa atatangazwa muda wowote ndani ya siku
saba.
Kauli hiyo inayoibua maswali mengi
imekuja baada ya viongozi wa umoja huo waliofanya vikao hadi usiku jana
bila ya viongozi wakuu wa CUF ambao wameahidi kutoa msimamo wao leo saa
5.00 asubuhi.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia
alisema wamekamilisha mazungumzo ya kumpata mgombea wa urais ambaye
watamtangaza kwenye mkutano wa hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi
na viongozi wengine wa vyama hivyo alisema hakuna mpasuko kama
inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na naibu wake wa Bara, Magdalena Sakaya hawakuhudhuria kikao hicho kilichofanyika kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.
Badala yake, Sakaya aliiambia Mwananchi
jana jioni kuwa CUF haikuweza kushiriki kikao hicho kwa kuwa kulikuwa na
mambo ambayo hawajakubaliana ndani ya chama na kwamba kama wangemaliza
mapema, wangekwenda kwenye kikao hicho.
Baadaye usiku, CUF ilituma taarifa kwa
vyombo vya habari ikisema kuwa itazungumza na waandishi wa habari leo
saa 5.00 asubuhi kwenye ofisi za chama hicho Dar es Salaam kutoa taarifa
kuhusu Ukawa.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF jana na
habari kwamba chama hicho kitatoa taarifa peke yake leo, kunaweka giza
nene mbele ya vyama vinavyounda Ukawa; Chadema, CUF, NCCR Mageuzi na NLD, ambavyo vilikubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Kutokuwapo kwa viongozi wa CUF
kulisababisha Ukawa kushindwa kumtaja mgombea wake na habari ambazo
zilipatikana awali, zilisema huenda vyama hivyo vikatangaza jina la
chama kitakachotoa mgombea urais badala ya jina la mgombea.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho
zilisema hoja kubwa ilikuwa katika suala la mgombea urais, nafasi ambayo
inawaniwa na Profesa Lipumba ambaye ameshachukua fomu za CUF na Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye anaungwa mkono na vyama vyote vinne.
Tayari Profesa Lipumba ameshagombea
urais mara nne bila ya mafanikio, wakati Dk Slaa aligombea mwaka 2010 na
kushika nafasi ya pili, akiwa ameitikisa CCM iliyopoteza asilimia
takriban 20 ya kura za mwaka 2005.
Sakaya alisema jana kuwa CUF
haikushiriki kikao cha jana kutokana na kutoafikiana baadhi ya mambo
ndani ya chama chake, ikiwa ni pamoja na suala hilo la kusimamisha
mgombea mmoja wa urais kupitia Ukawa.


Note: Only a member of this blog may post a comment.