Na Haruni Sanchawa
TUKIO la abiria Mosha Mahona kuwajeruhi abiria wenzake watano aliokuwa nao ndani ya daladala lililokuwa gumzo wiki iliyopita jijini Dar, nyuma ya tukio hilo mapya yameibuka, Uwazi linakujuza. Tukio hilo lililotokea Julai 23, mwaka, Mosha alikuwa amepanda daladala hilo akitokea Posta kuelekea Ubungo Simu 2000, alipofika maeneo ya Jangwani akaanza kuwachoma visu abiria wenzake kisha na yeye kuuawa na abiria.
Akizungumza na Uwazi, mmoja wa majeruhi aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Andrew alisema katika vitu ambavyo vilimshangaza siku ya tukio, Mosha kabla ya kutekeleza unyama huo alikuwa ameshika kitabu cha dini kitu ambacho hakuna aliyetegemea kama angeweza kufanya tukio hilo.
“Yaani kila mtu alimuona ni mtakatifu, ghafla tulishangaa kuona anatoa kisu na kuanza kumchoma abiria mwenzetu aliyemsihi asichungulie nje wakati gari linatembea na mimi wakati najihami, alinichoma tumboni hadi utumbo ukatoka nje,” alisema Bakari.
Mbali na hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camilius Wambura ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, alisema wakati wakiendelea kumfanyia uchunguzi, walimkuta marehemu Mosha akiwa na vitambulisho vyenye majina tofauti.
“Kutokana na hali hiyo, licha ya kuwa mtuhumiwa ni marehemu, jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kupata historia ya maisha yake,” alisema Wambura.
Kama hiyo haitoshi, majeruhi mwingine wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Norman George ambaye alijeruhiwa mikononi, alisema amepewa taarifa na watu waliokwenda kumjulia hali katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa mtuhumiwa huyo ameshawahi kuhusishwa na matukio mengine ya namna hiyo.
“Nimeambiwa kuwa huyo marehemu Mosha si tukio lake la kwanza kuchoma watu visu, alishawahi kufanya lingine kabla ya hili hivyo huenda alikuwa na matatizo ya akili,” alisema Norman.
Andrew ambaye ndiye alijeruhiwa vibaya kiasi cha kupoteza fahamu kwa zaidi ya saa 19 katika tukio hilo, anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Muhimbili ambapo hali yake inazidi kuimarika.


Note: Only a member of this blog may post a comment.