Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa akionesha kadi ya Chadema mara baada ya kusajiriwa rasmi na chama hicho.
]HAKUNA adui wala rafiki wa kudumu
katika siasa. Huu ni msemo ulioasisiwa na mwanadiplomasia wa Israel,
Avil Primor ambaye amepata kufanya kazi katika nchi mbalimbali duniani,
ikiwemo ubalozi wa nchi yake nchini Ujerumani (1993-99) na katika Umoja
wa Ulaya (1987-91).
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia
urafiki kati ya nchi yake na Iran ulivyokuwa. Kabla ya mapinduzi ya
nchi hiyo ya Kiarabu ambayo ni taifa la Kiislamu mwaka 1979 yaliyomuweka
katika himaya Ayatollah Khomeini, wawili hao walikuwa ni marafiki wa
kufa mtu. Enzi hizo, Iran ilikuwa ni ardhi pekee kati ya mataifa yote ya
Kiarabu, ambayo yaliruhusu ndege za Israel kutua!
Leo, unapoitaja Iran mbele ya Israel ni
sawa na uhai na kifo. Ni maadui ambao kila mmoja anatamani mwenzake
ateketee mara moja. Lakini Primor, licha ya kusema hakuna adui wala
rafiki wa kudumu katika siasa, aliongeza kuwa kilicho cha kudumu kwa
wanasiasa ni masilahi yao!
Hilo ndilo tunalolishuhudia leo baada ya
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa anapokuwa sehemu ya
jeshi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kwa miaka
mingi, kimemtaja kama mmoja wa mafisadi wanaostahili kuogopwa katika
nchi hii.
Katika orodha ya watu hao waliotajwa, wapo wengine ambao pia wamehusishwa katika kashfa nyingine zilizohusu uporaji wa mabilioni ya shilingi za umma kwa kutumia nafasi zao za kiuongozi walizopata kuzishikilia siku za nyuma au hadi sasa wakiwa katika ofisi za umma.
Akiwa serikalini, tangu enzi za Rais William Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, Lowassa alikuwa mmoja wa viongozi wa juu waliokuwa wakitoa maneno mengi ya kejeli, kashfa na dharau kwa vyama vya upinzani vilipojaribu kwa namna yoyote, kuhatarisha neema za wakubwa wa chama na serikali.
Na Chadema, kimejipatia umaarufu mkubwa kwa jamii ya wanyonge baada ya kuonesha kuwa ni chama chenye nia ya kupambana na ufisadi na kutowajibika kwa viongozi wa umma, kiasi kwamba idadi kubwa ya wafuasi wake ni watu waliokata tamaa na ambao kwa namna moja au nyingine, hawafaidiki moja kwa moja na uwepo wa CCM madarakani.
Uadui wa wawili hawa umemalizika. Leo Chadema wanamtaja Lowassa kama mchapakazi aliyeathiriwa na mfumo wa kifisadi ndani ya CCM na mbunge huyo wa Monduli, anaamini chama chake kipya ndicho pekee kinachoweza kuwaondoa marafiki zake wa siku nyingi madarakani.
Uadui na urafiki unaweza kumalizika wakati wowote, lakini masilahi ya wanasiasa daima huwa ya kudumu. Lengo la Chadema (Ukawa) ni kushika dola, bila kujali inashirikiana na nani na ndivyo pia ilivyo kwa Lowassa, kwamba hamu yake ni kukalia kile kiti cha enzi pale magogoni, bila kujali anafikaje.
Nia yangu hapa ni kujaribu kuwaweka sawa wafuatiliaji wa safu hii, kama nilivyopata kuwapa dokezo wiki iliyopita kuwa wanatakiwa kuwa macho sana na wanasiasa kwa sababu hawaaminiki.
Wanachokisema hakitoki ndani ya mioyo yao, isipokuwa kinatokana na wakati wenye kuhusisha masilahi yao.
Kwa kuwa Lowassa ana watu wengi nyuma yake wanaoweza kuwasaidia Ukawa wakaingia Ikulu, hawana shida kuungana naye, hata kama miongoni mwao, watakuwa ni walewale waliotajwa Septemba ile, pale uwanja wa Mwembeyanga, mwaka 2007.

Note: Only a member of this blog may post a comment.