Kuchimba na kusoma vitabu vyao mbalimbali kwa takriban miaka mitatu nilijifunza kuwa Freemasons wa zama hizo walikuwa wakijikusanya kama kikundi cha ushirika ili waweze kupata kazi husika. Walitambuana kwa salamu zao za siri na ishara mbalimbali zilizokuwa hazifahamiki kwa watu wengine.
Tukirudi nyuma, mwaka 1347 hadi 1351 baada ya Kristo, wakati Ulaya ikipambana na janga la Black Death (vifo vingi vilivyotokana na mlipuko wa magonjwa barani Ulaya katikati ya karne ya 14), mambo mengi yalikwenda mrama, taratibu na mipango mingi iliharibika, shughuli za ujenzi zilipigwa marufuku.
Freemasons ambao walikuwa na taaluma ya ujenzi hivyo walijikuta kwenye wakati mgumu.
Wakati Ulaya inapambana na Black Death, janga lililosababisha mabalaa mengi ikiwemo kwa jumuiya mbalimbali kupigwa marufuku kabisa au kunyimwa kufanya kazi katika utaratibu waliouzoea, takriban miaka 70, kabla ya Black Death, sehemu fulani ya Ulaya ilikumbana na kitimutimu kingine ambacho athari yake iliyosubiriwa kwa takriban miaka 70 iliweza kuonekana.
Athari ya kile kilichotokea, sehemu fulani nchini Ufaransa, ilisubiri mpaka balaa la Black Death lilipokuja na fursa mpya ambayo kwayo, Freemasons wa leo walianza rasmi.
Tukijikita barani Ulaya, Jumuiya ya Freemasons ya Kiingereza (English Freemasons) imekuwepo kwa zaidi ya miaka 300 sasa huku ikiwa na wanachama maarufu kama wafalme, wana wa wafalme, mawaziri wakuu, viongozi wa dini, wafanyabiashara wakubwa, wanasayansi, wacheza filamu, wanamuziki na hata waandishi.
Jumuiya ya Freemasons ilitia nanga katika Afrika ya Mashariki mwaka 1904 na mahali pa kwanza pa mkutano ilikuwa ni Zanzibar.Kipindi hicho ndicho ambacho Freemasons walianza kushamiri Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla na kwa wakati wote huo wameshawahi kutembelewa na watu kadhaa maarufu akiwemo Rais wa 26 wa Marekani, Theodore Roosevelt mwaka 1909 huku ziara yake ikielezwa kuwa ya ‘binafsi’.
Mwingine aliyewahi kufika Afrika Mashariki ni Arthur George ambaye baadaye alikuwa Mfalme George VI wa Uingereza, baba wa Malkia Elizabeth II na wengineo kadhaa.
Kiongozi mwingine wa English Freemasonry ni jamaa aliyetajwa kwa jina HRH Duke wa Kent ambaye ni binamu wa Malkia Elizabeth II. Inaelezwa kuwa kuna wanachama wapatao 3,000 wa Freemasonry katika nchi za Kenya, Uganda, Tanzania na Visiwa vya Shelisheli ambao kwa muda mrefu walikuwa chini ya kiongozi wao, Sir Jayantilal Chande ambaye hata hivyo ameshastaafu.
Makao makuu ya Freemasons ambayo kimsingi yamesajiliwa na Msajili wa Vyama (Registrar of Societies) yapo jijini Nairobi, Kenya katika Barabara ya Nyerere.
Kwa hapa Tanzania wengi wanafahamu ilipo loji (lodge) ya Freemasons pale Barabara ya Sokoine, Posta jijini Dar nyuma ya Majengo Pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Orodha ya Freemasons maarufu ni ndefu sana. Baadhi yao ni HRH Prince Philip, Duke wa Edinburgh, mume wa Malkia Elizabeth II, marais 14 wa Marekani wakiwemo George Washington, Franklin D. Roosevelt, Theodore Roosevelt, Harry Truman, Gerald Ford, George Bush, Ronald Reagan na Bill Clinton.
Pia katika orodha kuna viongozi mashuhuri kama Jenerali Colin Powell na MacArthur, Cecil Rhodes, Olof Palme, Ted Kennedy, Francois Mitterand, Napoleon Bonaparte, Winston Churchill, Willy Brandt, Robert McNamara, Edger Hoover na Tony Blair.
Katika orodha hiyo unapata watu kadhaa mashuhuri kwenye tasnia tofauti wakiwemo viongozi wa dini kama Swami Vivekananda, askofu mkuu wa zamani wa Canterbury, Rev. Geoffrey Fisher, wanaharakati kama Jesse Jackson, wafanyabiashara kama Fords, Rothschilds na Rockefellers na Richard Wagner. Watu kama Mozart, Shakespeare, Rudyard Kipling na Alexander Fleming pia ni kati ya Freemasons maarufu. Hata Neil Armstrong, mwanadamu wa kwanza kutua kwenye mwezi anatajwa kwenye listi hiyo.
Je, utajiri wao unatokana na nini na je, wana mchango gani katika jamii? Usikose kila Jumatano katika gazeti hili la Risasi Mchanganyiko. Kwa maoni tuwasiliane kwa namba hiyo hapo juu.

Note: Only a member of this blog may post a comment.