Musa Mateja na Imelda Mtema
Ule usemi wa kwamba
milima haikutani, binadamu hukutana umejidhihirisha baada ya staa wa
Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, kukutana uso kwa uso na aliyekuwa
mchumba’ke, Penniel Mwigilwa ‘Penny’ kwenye shughuli ya 40 ya mtoto wa
mwigizaji, Aunt Ezekiel hivyo kupata fursa ya kukumbushia enzi zao.
Aliyekuwa mchumba’ke Diamond Penniel Mwigilwa ‘Penny’.
Tukio hilo lililoshuhudiwa na Ijumaa Wikienda lilijiri wikiendi
iliyopita nyumbani kwa Aunt, Mwananyamala, Dar ambapo pati hiyo
ilihudhuriwa na mastaa kibao.
Katika tukio hilo, Diamond ndiye aliyeanza kumuona Penny akamwita kwa
lengo la kumsalimia ambapo naye alitii akionekana mwenye furaha kisha
walikumbatiana huku baadhi ya waalikwa wakiwataka kukumbushia enzi za
mapenzi yao.
Baada ya salamu, waliendelea kuzungumza ‘mambo yao’ huku muda wote wakicheka.
Baadaye, Penny aliwasalimia baadhi ya watu waliokuwa wamekaa na Diamond
na kwenda kukaa pembeni yao huku akitazamana na Diamond kwa shauku
kubwa.
Ijumaa
Wikienda liliendelea kufuatilia kila jambo juu ya wawili hao ambapo
muda mwingi walikuwa wakitaniana huku Romy Jones akichagiza utani
huo.Hata hivyo, baadaye Romy alinyanyuka alipokuwa ameketi na kwenda kwa
Penny kama mtu aliyeagizwa jambo na Diamond ambapo walizungumza kwa
kirefu.
Alipoulizwa
Penny kulikoni yeye na Diamond kuwa gumzo mahali hapo, alisema kuwa
hana sababu ya kununa maana hakuna kibaya ambacho kipo kati yake na
jamaa huyo kwani wamekuwa wakiwasiliana na kuongea vizuri ingawa kila
mtu ana mambo yake.
“Hapa tumealikwa na kila mtu amekuja kivyake, sasa si rahisi ukawaona
watu usiwasalimie au uchukie maana hakuna sababu ya kufanya hivyo, sina
ugomvi na Diamond na sina mipaka yoyote ya kusalimiana au kuongea
naye,” alisema Penny.
Kwa
upande wa Diamond alisema kuwa alikuwa pale kwa ajili ya kufuturu na
kumfurahia kila mtu hivyo hakuna dhambi yoyote kwake kusalimiana na
Penny.
Note: Only a member of this blog may post a comment.