KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Willibroad Slaa, (pichani) ambaye amekuwa ni kama alama ya chama hicho, anaweza kuwa ndiyo mwisho wake kufuatia ujio wa Edward Lowassa aliyejiunga Jumanne iliyopita na jana kuchukua fomu ya kuwania urais kupitia Chadema jijini Dar es Salaam.
Edward Lowassa na baadhi ya viongozi wa Chadema.
Dk. Slaa alionekana katika picha
iliyopigwa Jumapili usiku wakati wa Kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho,
ambayo pia ilimuonesha Lowassa akiwa amekaa pamoja na wajumbe hao
katika meza kuu. Siku hiyo ilidaiwa kuwa alikuwa akitambulishwa kwa
wajumbe hao. Wakati kukiwa na taarifa za kuwepo kwa mvutano kati ya
wajumbe wa Kamati Kuu, ambazo zinamtaja Dk. Slaa kuongoza wanaokataa
ujio wa aliyekuwa kada mkongwe wa chama tawala, Jumanne iliyopita,
ambayo Lowassa alitambulishwa rasmi mbele ya wanahabari, katibu huyo
mkuu hakuwepo sambamba na Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na
Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu.
SLAA, MNYIKA NA LISSU
Dk. Slaa, Mnyika na Lissu kwa miaka
mingi walikuwa mstari wa mbele katika kumshambulia Lowassa kwa tuhuma za
ufisadi na kutokuwepo kwao siku ya utambulisho huo, kulitajwa kama
dalili za mpasuko unaodaiwa kuwepo ndani ya chama hicho kikubwa cha
upinzani Tanzania Bara.
Inadaiwa Dk. Slaa haridhishwi na namna
chama hicho alichokifanyia kazi kubwa hadi kukubalika miongoni mwa
Watanzania, jinsi kilivyompokea pasipo masharti anayodaiwa kutaka
yafuatwe na Chadema kuelekea kumpokea kwake.
Dk. SLAA KAJIUZULU?
Wakati gazeti moja (siyo la Global) jana
liliripoti kuhusu kujiuzulu kwa kiongozi huyo aliyegombea urais mwaka
2010 na kuleta ushindani mkali kwa mshindi Rais Jakaya Kikwete, msemaji
wa chama hicho, Tumaini Makene aliliambia gazeti hili kuwa habari hizo
ni uzushi na kwamba Dk. Slaa alikuwa bado ofisini akiendelea na majukumu
yake ya kawaida.
Alipoulizwa kwa nini hakuwepo katika
hafla ile muhimu ya utambulisho wa Lowassa, Makene alisema chama kina
shughuli nyingi, hasa wakati huu kikijiandaa kuelekea uchaguzi mkuu,
hivyo kiongozi huyo alikuwa katika kutekeleza majukumu mengine.
LOWASSA KUCHUKUA FOMU ZA URAIS
Hata katika tukio kubwa zaidi
lililotokea jana, la mbunge huyo wa Monduli kuchukua fomu ya kugombea
urais kupitia Chadema, Dk. Slaa hakuonekana.
Gazeti hili lilipata taarifa za kususa
kwa Dk. Slaa katika shughuli za chama hicho na kwamba tangu Jumanne
asubuhi alikuwa amejichimbia nyumbani kwake, Mbweni, nje kidogo ya Jiji
la Dar es Salaam.
NYUMBANI KWA DK. SLAA
Uwazi Mizengwe lilifika
nyumbani hapo na katika hali isiyo ya kawaida, ulinzi uliimarishwa
tofauti na siku zingine na waandishi wetu walipojitambulisha na kuhitaji
kuonana naye, waliambiwa jambo hilo halitawezekana.
“Mnaweza kurudi tu kwenu kwa sababu mzee
hataki kuonana na mtu yeyote kwa sasa,” mlinzi mmoja wa nyumba hiyo
aliyejitambulisha kwa jina la Boniface aliwaambia waandishi wetu, ambao
kuona hivyo, waliomba kuandika ujumbe mfupi kwenye karatasi ili umfikie,
wakiamini kwa ukaribu wao, wangekaribishwa.
Nusu saa baadaye jana (saa 4.30 asubuhi)
mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbushi, alitoka nyumbani hapo akiwa na
dereva wake ndani ya gari lake, lakini katika hali isiyo ya kawaida,
hakuweza kusalimiana na waandishi wetu ambao kabla ya jana, walikuwa na
uhusiano wa karibu wa kikazi.
Baada ya kukaa hapo kwa saa moja na nusu
zaidi, kiasi cha saa sita, watu ambao walinzi waliwaelezea kama ni
washauri wa Dk. Slaa walitoka nje ya geti na waandishi wetu walifanikiwa
kumuona kiongozi huyo akirejea ndani kwake baada ya kuagana na wageni
wake getini.
Hadi walipoondoka nyumbani hapo saa saba mchana, mwanasiasa huyo mwenye ushawishi hakuwa ametoka nje ya geti la nyumbani kwake.
MAKAO MAKUU YA CHAMA
Katika Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema,
zilizopo Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam, mwandishi wetu
aliwashuhudia viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwa katika
shamrashamra za kumsubiri Lowassa kuchukua fomu hizo za kuwania urais
kupitia chama hicho. Hata hivyo, Katibu Mkuu Dk. Slaa hakuwepo.
Baada ya Lowassa kuwasili ofisini hapo,
aliingia Ofisi ya Katibu Mkuu ambako habari zinasema alikabidhiwa fomu
hiyo kwenye uzio wa makao makuu na Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema,
Freeman Mbowe.
Katika tukio hilo la uchukuaji wa fomu,
mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu alikuwepo na hivyo kuondoa uvumi
kuwa naye alikuwa akimkwepa Lowassa.
Lakini katika hali ya kushangaza, baada
ya shughuli za uchukuaji fomu kumalizika, Lissu alipoulizwa kuhusu
kutoonekana kwa Dk. Slaa, alisema kuwa kiongozi huyo alikuwa ndani
ofisini kwake akiendelea na vikao.
Lakini alipoelezwa kuwa mwandishi wetu
alikuwa na mtendaji huyo wa chama nyumbani kwake, Lissu alikaa kimya na
baadaye akajiondoa mbele ya mwandishi wetu bila kufafanua lolote.
Habari zaidi zinasema, tagu ‘kususa’ kwa
Dk. Slaa, viongozi wa chama hicho wamekuwa na vikao vingi, vyote
wakipanga ni namna gani wanaweza kumshawishi kiongozi huyo kurejea
kundini.
Mipango hiyo inajumuisha kuundwa kwa
jopo la watu wenye kuheshimiana na Dk. Slaa ili kukaa naye kukabili
tatizo hilo, ambalo kama litathibitika kuwa kweli, linaweza kusababisha
kuyumba kwa chama hicho tishio kwa CCM. Jana, mitandao mbalimbali ya
kijamii ilisambaza habari kwamba Dk. Slaa amejiondoa ndani ya chama
hicho. Hata hivyo, hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuelezea uvumi huo.
Imeandikwa na Makongoro Oging, Haruni Sanchawa na Brighton Masalu.

Note: Only a member of this blog may post a comment.