Na Khadija Mngwai, Dar es Salaam
WAKATI wa usajili mambo mengi yanatokea, nyota wa Simba, Emmanuel Okwi amebakisha miezi sita tu kuitumikia timu yake na sasa anajadiliana na uongozi kuhusu kuongeza mkataba baada ya Yanga kumwambia: “Noo, haiwezekani.”
Okwi ambaye ametua Simba msimu uliopita akiwa na mvutano na Yanga kwa utata wa kuvunja mkataba wake, kwa sasa anajadiliana na viongozi wake ili kuongeza mkataba mapema kuepuka kuwa mchezaji huru hapo baadaye.
Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Usajili ya Simba, aliliambia Championi Jumamosi: “Okwi amebakiza mkataba wa miezi sita, sasa tunafanya naye mazungumzo kwa ajili ya kuongeza mkataba mwingine kabla ya huu wa awali kufikia tamati.”
“Mambo yakikaa vizuri muda wowote kuanzia sasa Okwi atasaini mkataba mpya kwa mujibu wa makubaliano na wala hakuna tatizo.”
Simba inaonekana kujifunza kwa kosa lililofanywa na Yanga na Mbeya City kwa kuruhusu wachezaji wake kujiunga na timu nyingine wakiwa huru baada ya kumaliza mikataba yao. Ngassa wa Yanga amejiunga na Free State Stars ya Afrika Kusini kama mchezaji huru wakati Mbeya City imewaacha Deus Kaseke akijiunga na Yanga, Peter Mwalyanzi akitua Simba wote wakiwa wachezaji huru.


Note: Only a member of this blog may post a comment.