Tuesday, June 23, 2015

Anonymous

UKIWA HIVI, HAKIKA MAPENZI KWAKO YATA ‘RANI’ DUNIA!

NI Jumanne tena, naamini wapenzi wasomaji wa safu hii mpo sawasawa kabisa kimawazo na kivingine! Mada ya leo ndiyo hiyo; ukiwa hivi, mapenzi kwako yata ‘rani’ dunia! 
Kwanza ni hakika pasipo na shaka kwamba, sehemu kubwa ya vifo duniani vinatokana na mapenzi kwa namna moja au nyingine. Uhusiano katika jamii kuvurugika kisa ni mapenzi. Wanandugu kugombana, mapenzi yanachangia. Mambo mbalimbali yayowapata wanadamu, mapenzi ni sababu.


KWA NINI?
Nimekuwa nikifuatilia kwa undani visa mbalimbali katika jamii na kubaini kwamba, watu wengi, hasa wanaume, kujituma kwao kutafuta pesa ni ili baadaye wawe  na maisha mazuri lakini mara nyingi ni kwa sababu ya pesa hizo kufanyia starehe.
Hamis Muuzangi, mkazi wa Tip Top, Dar niliwahi kuzungumza naye akiwa kwenye sehemu yake ya kazi, Mwenge kuhusu juhudi zake za kusaka pesa zinatokana na nini hasa, alisema:
“Kaka hakuna kingine, najituma kwa pesa ndogo sana, siwezi kujenga nyumba lakini naweza na mimi jioni kukaa kwenye ‘kiti kirefu’ (baa) ili kupata bia mbili huku watoto wazuri ‘mademu’ wakipita mbele yangu. 

“Unajua mwanaume yeyote rijali, akipata pesa lazima atazila na mwanamke aliyempenda. Mfano mimi, siku sina pesa, sipokei kabisa simu ya demu wangu. Siku nikiwa nazo, namtafuta mwenyewe ili tukae kivulini.” 

KUBURUDISHA MOYO
Muuzangi aliendelea kusema kuwa, anapokuwa na demu wake baa wakitumbua maisha, hata uchovu wa kazi huondoka tofauti akiwa peke yake au na washkaji zake.
“Unajua mwanamke ni mwanamke tu. Ukikaa naye mahali, mwanaume unajiona wewe ni bora zaidi. Asikudanganye mtu kaka, hata msukuma mkokoteni, mbeba zege, ombaomba, ikifika jioni anapenda kuwa na mwanamke anayempenda.” 

VIFO VYA MAPENZI
Kuna baadhi ya vifo vimekuwa vikisemwa chanzo chake ni mapenzi. Mfano, wivu! Tumekuwa tukisoma kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba, mwanaume kamuua mkewe kisa wivu wa mapenzi. Kwamba, kamfumania na mwanaume mwingine. 

Pia, wapo waliosemekana wamepoteza maisha kwa sababu eti walitupiwa magonjwa ya ajabu. Hii huwapata zaidi wanawake, kwamba anafanyiwa ukatili huo kwa vile alimchukua mume wa mwenzake. Wapo wanaopoteza maisha kwa njia ya kujinyonga, hasa wanaume! Kisa? Walijitolea kusomesha wanawake, baadaye wanawake hao wakapata kazi nzuri na kuamua kuwa na wanaume wengine, hasira zikaanzia hapo. 

Wapo waliodiriki hata kutumia silaha kama bunduki au bastola, kwa kuwatoa uhai wote. Mume anamfumania mkewe, anaamua kuua mke na mgoni wake! 

KUVURUGIKA KWA UHUSIANO
Ukiachana na vifo, mapenzi pia yamekuwa yakichangia kwa sehemu kubwa kuparaganyika kwa uhusiano mwema.
Utakuta Neema anataka kuolewa na John, lakini wazazi na baadhi ya ndugu wa Neema hawamtaki John. Matokeo yake, Neema kwa vile msimamo wake ni huo, anaamua kufanya mambo yake kwa nguvu kwa kutumia ndugu wachache wanaomuunga mkono bila kujali uhusiano wake na wazazi wake au ndugu. 

Hii hutokea hata kwa wanaume. Wazazi hawamtaki mchumba, mwanaume anaamua kufunga  naye ndoa bila ridhaa, matokeo yake mawasiliano mazuri ya awali yanatoweka kwa vile mwanaume alishapenda. 

Si hapo tu, wapo watu mitaani wamevurugana kisa, mtoto wa kiume wa mzee  Mohamed amebainika kutembea na binti wa mzee Mwaijande, wazazi wanaingia kwenye bifu la moja kwa moja. Hakuna salamu wala kutembeleana kama zamani. 
Mada hii ndiyo kwanza imeanza. Uchambuzi zaidi utaendelea wiki ijayo ili kujua watu ambao mapenzi yana ‘rani’ dunia kwao. Usikose!

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.