MWADUI FC ya Shinyanga haitaki mchezo na imesema tayari imemsajili beki wa kati David Mwantika aliyemwagwa Azam FC, usibishe.
Timu hiyo iliyopanda daraja na kupata tiketi ya kucheza msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kama ilivyo kwa African Sports, Toto African na Majimaji, imetamba kwa usajili huo wa Mwantika lazima itishe.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mwenyekiti wa Mwadui, Omary Khatibu, alisema kila kitu kimeenda sawa na tayari wameshakamilisha usajili wao kwa kumnasa Mwantika.
“Tumeshamalizana na Mwantika ambaye tunaamini atatusaidia kwani ni chaguo la kocha wetu (Jamhuri Kihwelo ‘Julio’),” alisema Khatibu.Hadi sasa Mwadui imefanya usajili wa baadhi ya wachezaji ambao ni Malegesi Mwanga na Rashid Mandawa kutoka Kagera Sugar, Shaaban Kado (Coastal Union), Nizar Khalfan (Yanga), Zahoro Pazi (Huru) Paul Nonga na Antony Matogolo kutoka Mbeya City. “Kama mipango itabadilika na kuwa na ulazima wa kusajili wachezaji wengine basi tutafanya hivyo lakini kwa sasa tumemaliza kazi,” alisema Khatibu.

Note: Only a member of this blog may post a comment.