Tuesday, May 26, 2015

Anonymous

MSHTUKO! Ray Ashangazwa,Tuzo za TAFA!

LICHA ya Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) kufanikiwa kutoa tuzo za kwanza za TAFA, mwigizaji maarufu, Vicent Kigosi ‘Ray’, ameonyesha kutoridhishwa na uandaaji wa tuzo hizo.

Tuzo hizo zilitolewa juzi usiku katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, huku Ray akikosekana katika kipengele hata kimoja kati ya vilivyoshindanishwa.

Ray aliingia ukumbini hapo akiongozana na msichana wakiwa wamechelewa, ingawa walikuwa makini kufuatilia utoaji wa tuzo hizo.

Hata hivyo, kabla tuzo mbili za mwisho hazijatolewa, wawili hao waliinuka katika viti walivyokaa wakaondoka zao, huku wakionyesha kutokuridhishwa na zoezi hili.
Katika mazungumzo na baadhi ya waandishi wa habari, vipengele vilivyoonekana kumkera Ray na wahudhuriaji wengine ni cha Best AC kilichokuwa kikihusu mtu, kampuni au taasisi iliyotoa mchango mkubwa kwenye filamu.

“Sasa Best AC ndiyo tuzo gani hii?’’ aliuliza Ray na kuendelea; “Mbona kuna majina mengi ya kuita tuzo, lugha yenyewe iliyotumika ni Kiingereza, mtu anaelewa kweli hiki kipengele bila ufafanuzi,” alilalama Ray, huku akiondoka ukumbini hapo.
Ray aliongeza: “Tuzo ni nzuri, ingawa sipo kwenye kipengele chochote kwa kuwa Watanzania ndio wameamua, nakubaliana na maamuzi,’’ alieleza.

Akifafanua kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa waandaaji wa tuzo hizo, Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifamba, alisema wanastahili pongezi kwa kuwa hawakuwa na wadhamini wakubwa, lakini wameweza kuendesha zoezi hilo kwa mafanikio.

“Changamoto lazima ziwepo, kwa kuwa ndiyo tunaanza, tunaomba Watanzania watuunge mkono ili mashindano haya yafike mbali, kwa kuwa kwa sasa tunatumia fedha zetu wenyewe na misaada midogo kutoka kwa washirika wetu, kwa hili la lugha tumelazimika kutumia Kiingereza kwa kuwa tumeshindwa kupata fasili ya neno la Kiswahili, lakini pia kulikuwa na wageni mbalimbali, imesaidia kujitangaza na kuongeza ufahamu,’’ aliendelea.
-Mtanzania

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.