Tuesday, May 26, 2015

Anonymous

KWA TUHUMA HIZI, LOWASSA NJIA NYEUPE KUELEKEA IKULU OKTOBA 2015

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa.
MOJA kati ya mambo wananchi wanatarajia kusikia katika vyombo vya habari ni kuhusu wagombea urais, hasa wale ambao tayari wameshatangaza nia ya kuwania kiti hicho, ni taarifa mpya kuhusu wao. Kwa lugha nyepesi ya msimu tunaweza kusema “habari ya mjini kwa sasa.” 

Hiyo inatokana na ukweli kwamba baada ya baadhi ya wagombea kufungiwa kujihusisha na ushawishi wa kisiasa kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kile kinachodaiwa kwamba kuanza kujihusisha na kampeni za kusaka uungwaji mkono wa kuwania urais kinyume na kanuni na taratibu za Chama Cha Mapinduzi, (CCM). 

Waliokuwa wakitumikia adhabu hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje ambaye ameshaaga Wizara yake, Bernard Membe, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye. 

Katika kipindi hicho cha kifungo, makada hao hawakuruhusiwa  kujihusisha na shughuli zozote za  kisiasa zenye mwelekeo wa kampeni. Waliondolewa kifungo hicho baada ya Kamati Kuu ya CCM wiki iliyopita, kuridhia mapendekezo ya Kamati Ndogo ya Maadili iliyokuwa ikiongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula ili kuwaondoa kifungoni.
Bila shaka hiyo ilikuwa habari njema kwao, kwa kuwa ndicho walichokuwa wakisubiri kwa hamu.

Baada ya kifungo hicho, wanasiasa hawa hivi sasa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba wanacheza karata zao za mwisho ili waongeze ushawishi katika ngazi zote za chama hasa kwa upande wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), na Kamati Kuu, ili kupenya katika uteuzi wa kuwania urais kupitia chama tawala (CCM). 

Ikiwa ni siku moja tu baada ya adhabu ya kifungo kumalizika, Lowassa anatarajia kukutana na wahariri leo mjini Dodoma kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ya kisiasa. Huu ni mkakati ambao anaamini unaweza kumpa nguvu zaidi kisiasa hasa wakati wa uteuzi wa mgombea wa kiti hicho ambao hautabiriki ndani ya chama hicho. 

Kwanza niseme tu kwamba kutokana na ajenda zitakazojadiliwa kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waandaaji wa mkutano huo wa Lowassa, ni dhahiri kuwa mwanasiasa huyo ametafakari kwa kina kuhusu njia mwafaka za kujisafishia njia katika safari yake ya kuelekea ikulu. 

Lowassa ameamua kumaliza sintofahamu za kisiasa ambazo zimekuwa zikijadiliwa juu yake, bila kujibu lolote.
Katika hili nadhani, Lowassa alishauriwa vizuri na wapambe wake akaamua kutumia mbinu ya kukaa kimya kwa kipindi chote huku akiamini kuwa lawama nyingi juu yake hazina mashiko. Sitaki kumsemea lakini nadhani mantiki ya mkutano wa leo na wahariri ni kupangusa matope yote yliyomchafua kisiasa. 

Kwa kujibu wa taarifa ya mkutano huo, mambo atakayoyazungumzia leo ni pamoja na kashfa ya uagizaji wa mitambo ya kufua umeme na Kampuni ya Richmond ambayo ilimwondoa madarakani kwa kuamua kujiuzulu. Katika hili, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu, atatoa ufafanuzi kama alihusika, hakuhusika ama alisingiziwa kwa lengo la kumchafua kisiasa. 

Aidha, atazungumzia kuhusu utajiri wake unaohusishwa na umiliki wa mali nyingi wa kutisha ndani ya nchi, uhusika wake katika harambee mbalimbali anazoshiriki hasa katika nyumba za ibada za madhehebu mbalimbali ya dini na kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi makubwa ya fedha yanayodaiwa kufanywa na wafuasi wake kushawishi baadhi ya makundi mbalimbali ya kijamii kumuunga mkono katika harakati za kuwania urais. 

Hayo ni baadhi tu kwani naamini kuwa katika mkutano huo, yapo mengi yatakayoulizwa kutokana na yatokanayo na mkutano huo.Nina uhakika kuwa katika mkutano wa leo, Lowassa anayo majibu ya kutosha kutokana na tuhuma nyingi zilizokuwa zikimkabili. 

Si kwamba siku zote hakuwa na majibu, lakini aliamua kuzitumia kama mtaji wake wa kisiasa kwa kipindi hiki. Ukitafakari utaona kwamba iwapo angeyazungumza mapema haya anayotaka kuzungumza angepata wapi ‘political kick’  katika vyombo vya habari. Niwaulize wahariri kwamba kesho nani anaweza kuacha habari ya Lowassa?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.