Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi.
Nassor Gallu,Dar es Salaam.KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mganda, Emmanuel Okwi, ameweka wazi kuwa alitaka kupiga penalti ambayo Ibrahim Ajibu alipiga na kukosa juzi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Katika mchezo huo ulioisha kwa Simba kushinda mabao 3-0, Simba walipoteza penalti katika dakika ya 12 baada ya Ajibu kuupaisha mpira juu ya lango la Ndanda.
Simba walipata penalti hiyo baada ya Okwi kuangushwa na Kassian Ponera. Mganda huyo alichukua mpira na kuuweka eneo husika akitaka kupiga, lakini Ajibu alifika eneo hilo na kuutenga, hivyo Okwi kuishia kurusha mikono na kukaa pembeni akikubali yaishe.
Okwi alitaka kupiga kwa kuwa yeye ndiye mchezaji wa Simba mwenye mabao mengi, hivyo kufunga penalti hiyo kungemsaidia kusogea juu katika vita ya ufungaji bora.
Mara baada ya mchezo huo, Okwi mwenye mabao 10 mpaka sasa katika ligi kuu, aliliambia Championi Jumatatu kuwa, alitamani kupiga penalti hiyo ili kuongeza mabao kama angefanikiwa kufunga, lakini akasisitiza hata kupiga Ajibu hakuna tatizo kwa kuwa ni utaratibu wa timu na lengo lao ni moja, kuisogeza Simba ili kumaliza nafasi ya pili mwishoni mwa msimu.
“Kweli nilitaka kupiga penalti ile, lakini haikuwa hivyo, nilimwachia Ajibu kwa kuwa ndiyo huwa anapiga mara kwa mara na anapatia sana ingawa leo (juzi Jumamosi) amemisi.
“Kwa upande wangu kilichonisikitisha ni Ajibu kukosa penalti na si vinginevyo, kwa sababu kama ufungaji bora bado tuna michezo miwili mbele, kwa hiyo ninaweza kufunga na kumfikia aliye juu,” alisema Okwi aliyezaliwa siku ya Krismasi mwaka 1992.


Note: Only a member of this blog may post a comment.