Wednesday, April 8, 2015

Anonymous

LIGI KUU BARA: Yanga, Azam ni vita ndani na nje ya uwanja!

Dar es Salaam. Waswahili husema, hakuna kulala hadi kieleweke. Hivyo ndivyo unavyoweza kuzungumzia mbio za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambazo dhahiri zimekuwa za Yanga na Azam.

Mbio hizo zitaendelea leo  kwa Yanga kuikabili Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Azam ikiialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Timu hizo zinafukuzana  kuwania ubingwa ambao mbio zake zimegeuka vita nyingine kali ambayo mshindi wake atasaidiwa zaidi na mbinu pia matokeo mazuri kwenye mechi zilizosalia kabla ya kumalizika kwa msimu.

Vita nyingine ni  ya kusaka tuzo ya mfungaji bora kati ya Simon Msuva wa Yanga na Didier Kavumbagu wa Azam.

Tayari, Msuva amefunga mabao 11, akifuatiwa kwa karibu na Kavumbagu,  mwenye mabao 10 sawa na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar katika orodha ya wafungaji bora.

Kavumbagu amekuwa na wastani mzuri wa kufunga bao kila mechi kwa siku za karibuni,  tofauti na  Msuva ambaye mara nyingi amekuwa akipoteza nafasi nyingi za kufunga.

Kabla ya mechi za leo, Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 40, ikifuatiwa na Azam iliyoko katika nafasi ya pili, ikiwa na pointi 36, ingawa  ina mchezo mmoja mkononi.

Yanga inaikabili Coastal ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza kwa bao 1-0, hivyo itaingia uwanjani ikijiamini kutaka kuendeleza rekodi yake nzuri nyumbani.

Kocha Hans Pluijm amekiri kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na uimara wa wapinzani wao, lakini akieleza kuwa wamejipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo na mingine iliyobakia ili kutwaa ubingwa.

Mholanzi huyo alisisitizia wachezaji wake kuwa hawana budi kuzitumia nafasi wanazopata kwani wao ndio chanzo cha kuinyima timu yao ushindi wa mabao.

“Ninachosisitiza ni wachezaji wangu kutumia nafasi wanazopata, timu imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi, lakini umakini wa washambuliaji wangu umekuwa mdogo, hivyo wanahitajika kuongeza umakini ili tupate mabao mengi,” alisema Pluijm.

Kocha wa muda wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema, wamejiandaa na hawana hofu na Yanga kwani ni kama timu nyingine yoyote,  hivyo watu wasubiri kuona soka.

Azam watakuwa na kibarua kigumu kwa Mbeya City, wakijua kuwa kupoteza mchezo huo ni kujiweka katika hatari ya kukosa kushiriki mashindano ya Afrika mwakani

Timu hiyo ipo kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 36, inafuatiwa kwa karibu na Simba,  yenye pointi 35, ingawa imecheza mechi mbili zaidi, hivyo matokeo mengine zaidi ya ushindi kwao ni balaa.

Timu hiyo  itabebwa na rekodi katika mchezo huo kwani katika michezo mitatu waliyokutana na Mbeya City tangu msimu uliopita,  imeshinda michezo miwili na kutoka sare mmoja.

Pia, mwendo wa kusuasua wa Mbeya City msimu huu unaweza kuipa kazi rahisi Azam kupata ushindi,  ingawa hata hivyo mechi baina yao huwa haitabiriki.

Kocha George Nsimbe alisema anajua kuikabili Mbeya City ni kazi ngumu kwani wapinzani wao wanacheza soka la nguvu,  lakini wamejipanga kushinda.

Juma Mwambusi wa Mbeya City ambaye timu yake ililazimisha sare ya bao 1-1 na Ndanda wiki iliyopita, alisema dakika 90 ndizo zitaamua mshindi, hivyo ni jambo la kusubiri.
Hata hivyo, Mwambusi alieleza faraja ya kurejea kwa beki wake aliyekuwa amefungiwa mechi nane, Juma Nyoso akieleza kuwa kumempa faraja.
-MWANANCHI

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.