Friday, April 17, 2015

Anonymous

HUU NDIO UKWELI: BADO SIJAMUONA MSHINDI NDANI YA CCM!

Katibu Mkuu wa chama tawala (CCM), Abdulrahman Kinana.
NCHI ipo katika vuguvugu la uchaguzi mkuu, ambao data za awali zinasema utafanyika Oktoba 25, mwaka huu. Ni takriban miezi sita na ushee kuanzia sasa. Kwetu sisi wapigakura, ni muda mrefu umebaki, lakini kwa wanasiasa na wakubwa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), muda ni kama hautoshi. 

Ingawa tunaambiwa kuwepo kwa mgogoro ndani ya vyama vya upinzani, hasa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) juu ya nani atagombea kiti gani, lakini tishio la mgogoro mkubwa zaidi unaoweza kutishia ustawi wa taifa letu, upo ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). 

Hii ni kwa sababu hiki ndicho chama kilichoshika dola tangu tupate uhuru. Upo ukaribu mkubwa wa kiutendaji kati ya viongozi wa CCM na serikali na hili haliwezi kutenganishwa kwa namna yoyote. Mkubwa ndani ya chama, ni mkubwa serikalini, ingawa kinadharia tunaambiwa serikali haifungamani na vyama vya siasa. 

Mbele ya hadhara, wakubwa wanaweza kubisha juu ya kuwepo kwa mgogoro, lakini ndani ya nafsi zao, wanatambua kuwa CCM haiko sawa, imegawanyika makundi. Ndiyo, Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete nisimsemee, lakini kuna kundi la Edward Lowassa, la Bernard Membe, la Samuel Sitta, la Steven Wassira, la Mark Mwandyosa, la Emmanuel Nchimbi, la January Makamba na wengine wote wanaotajwa. 

Na ukumbuke, ninaposema hawa watu wana makundi yenye wafuasi, sizungumzii wafuasi njaa waliopo mitaani, wanaopiga kelele ili wapate hela ya mlo mmoja na bia, nazungumzia wafuasi ambao wana dhamana ndani ya serikali yetu, wana nafasi katika taasisi zetu nyeti, wana mamlaka katika maeneo tunayoishi. 

Ni watu ambao wanaweza kuamua lolote, wakati wowote, ilimradi tu kuonyesha furaha au hasira ya kufanikiwa au kutofanikiwa kwa makundi yao katika siasa ndani ya CCM. Kama kuna mtu hajui, makundi haya yana wafuasi ndani ya majeshi yetu, idara zetu za usalama na hata majaji na mahakimu. 

Ninafahamu, makundi ndani ya chama kimoja cha siasa wakati wa uchaguzi ni jambo la kawaida na hii imekuwepo kwa miaka mingi. Lakini tofauti na mara zote, safari hii katika Chama cha Mapinduzi, kilichopo ni uhasama wa kikwelikweli baina ya makada wake. 

Kuna uadui wa wazi kati ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu, Nape Nnauye na wafuasi wa Edward Lowassa ambao wanaamini yeye ndiye kinara wa kumpiga vita mbunge huyo wa Monduli katika harakati zake za kukamata dola. Kama ikatokea Mheshimiwa Lowassa akakatwa, kwenye ngazi yoyote, mtu wa kwanza kunyooshewa kidole atakuwa mwanasiasa huyu kijana, ingawa uhalisi hauonyeshi nguvu zake katika suala kubwa kama hilo! 

Wote hao, kwa sababu zao, wanatafuta ushindi ili kuiwakilisha CCM katika ‘shindano’ la Oktoba. Sijui wenye kambi zao, lakini uhasama unaojengwa hivi sasa katika harakati za uchaguzi mkuu ujao, siuoni kama utampa ushindi mtu yeyote, badala yake, natabiri mtifuano mkubwa chamani! 

Wanasema CCM ni bingwa wa kuvunja makundi mara baada ya uchaguzi ni sawa, kwa sababu imefanya hivyo mara nyingi, lakini mwendo wa safari hii, hauoneshi kama kuna mshikamano ule tuliouzoea. Kuna kuviziana, mazingira ya visasi na kujengeana hofu kusiko na sababu. Kila mtu anaangalia hatima yake endapo kundi flani litashinda! 

Ningepata nafasi ya kuongea na viongozi wakuu wa CCM, ningewashauri kuwaita makada wake wote wanaotajwa na wanaoutaka urais na kuzungumza nao. Waondoe kwanza tofauti baina yao kabla filimbi haijapulizwa ili kukijenga chama. 
Ni kujidanganya kuingiza timu mashindanoni ikidhani itashinda kwa hali kama hii, baadaye watu watakuwa tayari kusaidia kushindwa ilimradi tu kumkomoa adui y ao ndani ya CCM!

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.