Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi taifa, James Mbatia (wa pili kutoka kushoto), Mwenyekiti wa Chadema, Mhe Freeman Aikael Mbowe (wa pili kutoka kulia) na Katibu Mkuu wa Chama cha Chadema, Dk Willbroad Slaa (kulia).
VYAMA vinavyounda Umoja wa katiba ya Wananchi (UKAWA) leo vimetoa msimamo wao juu ya njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu unaotakiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.Ukawa imesisistiza kwamba kuahirisha kwa Uchaguzi Mkuu huo ni sawa na kumuongezea Rais Jakaya Kikwete na Chama chake cha Mapinduzi muda wa kuendelea kutawala Tanzania.
Ukawa imesema jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa kisingizio chochote kile kitakuwa ni kinyume na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msimamo wa UKAWA unafuatia kumalizika kwa kikao cha Viongozi Wakuu wa Vyama vinavyounda UKAWA kilichofanyika katika Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) jijini Dar kati ya tarehe 28 na 29 Aprili mwaka huu.
Akieleza msimamo wa UKAWA juu ya swala hili, Mwenyekiti wa Kikao hicho na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa kuna dalili za kuonyesha kwamba zipo njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu na kumuongezea Rais Kikwete Muda wa kutawala.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijaanza maandalizi yoyote kwa ajili ya Uchanguzi Mkuu licha ya kwamba imebaki miezi sita tu Uchaguzi huo ufanyike kwa mujibu wa Katiba.
Kwa upande mwingine, UKAWA imeitaka NEC kuakikisha kwamba wananchi wote wenye sifa ya kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanaandikiswa kwenye kwenye Daftari hilo.
Wakati huo huo, Viongozi Wakuu wa UKAWA wameeleza kushangazwa na taarifa zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kwamaba Chama cha NCCR- Mageuzi kimejitoa au kimeandika barua ya kuomba kujitoa kwenye UKAWA. Viongozi hao wamesema kwamba taarifa hizo ni za uzushi mtupu unaosambazwa na wapiga ramli kwa lengo la kuipatia CCM na Vyama vibaraka wake ahueni ya kisiasa.
Akikanusha taarifa hizo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi taifa, James Mbatia amesema kwamba yeye mwenyewe na Katibu Mkuu wake Mosena Nyambabe pamoja na maafisa wa chama chake wamekuwa katika hatua zote za vikao vya UKAWA kuanzia Kamati ya Ufundi na ile ya Wataalam hadi Kikao cha Viongozi Wakuu kilichomalizika jana.
Note: Only a member of this blog may post a comment.