Saturday, April 18, 2015

Anonymous

DONDOO Muhimu za Kufahamu Kabla Ya Mechi ya Yanga na Etoile du Sahel Pale Taifa Leo Alasiri

Waandishi wetu, Dar es Salaam
YANGA leo Jumamosi inacheza na Etoile du Sahel ya Tunisia katika Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.  Yanga  imeapa lazima Waarabu wakione cha moto. 

Katika mazoezi ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Karume, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm aliliambia Championi Jumamosi kwamba, atatumia soka la kasi kuimaliza mapema Etoile ambayo ina beki isiyo na kasi.
“Nimetazama video zao, mabeki wao hawana spidi hivyo nimewandaa mabeki wangu kuwamaliza mapema, najua joto la Dar es Salaam litawapa tabu,” alisema Pluijm. 

Amissi Tambwe aliyeugua Malaria na kiungo Salum Telela anayeumwa kifundo cha mguu, walionekana wakifanya mazoezi na wenzao kabla ya kuondolewa mwishoni na mambo yakiwa magumu kwa Telela basi Said Dilunga atacheza nafasi yake.
Hata hivyo, Daktari wa Yanga, Juma Sufian alisema: “Tutaangalia kesho (leo)watakavyoamka, kwani Tambwe na Telela kucheza kwao kutategemea zaidi na majaliwa ya Mungu.”
Alipozungumza na Championi Jumamosi, jana jioni Tambwe alisema; “Najisikia vizuri lakini itategemea na nitakavyoamka, lakini hali ikibaki hivi hivi nitacheza.” 

Akizungumzia mchezo huo, kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima alisema ana uhakika kikosi chao kitafanya vizuri dhidi ya Etoile kutokana na maandalizi waliyofanya.
“Tuna morali ya hali ya juu kushinda mechi ya kesho (leo) ukiachana na Tambwe na Telela wengine tupo tayari kwa mchezo huu, tumepania kufanya vizuri,” alisema Niyonzima.
Etoile mchecheto.

Mchezo wa leo utachezwa saa 9:00 Alasiri, katika mazoezi yake ya jana Ijumaa, Etoile ilifanya mazoezi kuanzia saa 9:30 mchana kwenye Uwanja wa Taifa lakini walionekana kutohimili hali ya hewa ya joto na kulazimika kusitisha propramu zao kila baada ya muda na kunywa maji. 

Wakati mazoezi hayo yakiendelea viongozi wa timu hiyo waliwafuata walinzi wa uwanjani hapo na kuomba wawafungulie milango ya vyumba vya kubadilishia nguo ili waweze kuviona vilivyo lakini walikataliwa. 

Hali hiyo ilionekana kuwaudhi Waarabu hao ambao walianza kulalamika wakibishana na walinzi hao ambao walikuwa makini na kazi yao.
Baada ya kukataliwa viongozi hao walirudi tena kwa mbinu nyingine wakisema wanaomba mapipa ili wajaze maji na barafu ili wachezaji wao waoge kupunguza joto mwilini, pia walikataliwa. 

Uchunguzi wa Championi Jumamosi ulibaini kwamba, Etoile walitaka mapipa hayo ili kuyaweka katika vyumba vyao vya kubadilishia ili hata kama vikipulizwa dawa ya kuwapunguza nguvu zisifanye kazi.
“Walidhani hatujui janja yao, walitaka mapipa ili wayaweke maji na kuyalaza hapa katika vyumba ili kupunguza nguvu ya dawa kama zikiwekwa,” alisema mmoja wa walinzi wa Uwanja wa Taifa.

USIPITWE! JIUNGE NASI FACEBOOK

Subscribe to this Blog via Email :

TOA MAONI YAKO HAPA (MATUSI HAYARUHUSIWI)

Note: Only a member of this blog may post a comment.