Huduma
ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka imeanza rasmi jana jijini Dar es
Salaam huku yakilalamikiwa na watumiaji wakiwemo baadhi ya watu
waliokuwa na msamaha wa kusafiri bila kutoa nauli, ambao sasa
hawatambuliwi na mfumo mpya.
Utaratibu uliokuwa umezoeleka awali wa askari wa polisi, jeshi, magereza na walimu kutolipa nauli kwenye usafiri wa daladala, umeonekana kugonga mwamba chini ya mabasi hayo.
Jana mwalimu ambaye hakufahamika jina lake alisikika akitaka mwongozo wa kutolipa nauli kwa kuwa yeye ni mwalimu.
“ Mama mfumo huu haumtambui mwalimu, askari,” alimjibu mmoja wa wahudumu wa UDA-RT aliyekuwa akihakiki tiketi za abiria kabla ya kupanda basi.
Akijibu
hoja hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa alisema mwongozo
uliotolewa na Sumatra, unamtambua mwanafunzi pekee ambaye anatakiwa
kulipa Sh 200, wengine wote wanatakiwa kulipa nauli.
Mbali
na walimu, askari, pia watu wenye ulemavu ambao walikuwa hawalipi nauli
kwenye daladala, kwenye mfumo wa mabasi yaendayo haraka wanatakiwa
kulipa.
Mambo
mengine yaliyolalamikiwa ni mfumo wa ukataji tiketi, ambao unadaiwa
kusababisha foleni ndefu huku wahudumu wakiwa hawana chenji, jambo
lililosababisha baadhi ya watu kulipa kiasi kikubwa cha fedha.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, baadhi ya abiria walisema walilazimika kukaa zaidi
ya dakika 20 vituoni kutokana na kusubiri chenji na wengine kuamua
kuacha fedha zao.
“Nimetoa
Sh 1,000, nimepewa tiketi na kurudishiwa Sh 200 na kuwa hana Sh 150.
Hapa inaonesha nimesafiri kwa Sh 800. Nauli hii ningeitumia kupanda
daladala na kuzunguka nalo ili nipate kiti, ningepandia upande wa pili
ningetumia Sh 500,” alisema Kasum Swakala, mkazi wa Ubungo Bonyokwa.
“Nina
haraka na siwezi kuipata hiyo 150 ambayo hawajanipa katika chenji
yangu, inabidi tu kuondoka ili kuwapisha wengine lakini hali hii
inatuumiza sana na siyo sawa kwa sababu kesho siwezi kurudi kuwadai
chenji yangu,” alisema.
“Nimetoka
Mbezi na kulipa 400, nimefika hapa wanasema hawana cheji kama nataka
nilipe 800, siwezi kulipa kiasi hicho naenda kupanda daladala.”
Meneja
Uhusiano wa UDA-RT, Deus Bugaywa alikiri kuwapo changamoto ya chenji na
kusema asubuhi walikuwa na chenji nyingi ambazo ziliisha haraka hivyo
kuleta usumbufu kwa baadhi ya abiria.
Mkazi
wa Mbezi, Laurence Msuya alilalamikia hatua ya kukata tiketi mara mbili
na kusema imesababisha usumbufu kwao kwa kupoteza muda. Wakala wa
kukatisha tiketi katika kituo cha Mbezi alilalamikiwa kuchelewa kufika
jambo lililozidisha msongamano.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya UDA-RT, David Mgwasa alisema hali hiyo itaondoka pale mfumo wa kadi utakapoanza kufanya kazi.
“
Wananchi tuliwafundisha namna ya kutumia kadi, na siku moja kabla
Serikali ikazuia matumizi yake, sasa tunasubiri maamuzi ili tuanze
kuuza. Tulijua wananchi wangekuwa na kadi na wale wachache ambao ni
wanafunzi na wale wanatumia mara moja moja ndio wangetumia tiketi za
karatasi,” alisema Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), John Shauri
Alisema mfumo wa tiketi za kadi uko katika hatua za mwisho na mazungumzo.
“ Ilikuwa ni lazima tuanze tiketi za karatasi, kwani tutakuwa na mifumo
miwili inayofanya kazi hii ya tiketi za karatasi na kadi, mambo
yakiwekwa sawa kadi zitaanza kutumika,” alisema.
Changamoto
nyingine katika huduma hiyo iliyofanywa na baadhi ya wakala wa
kukatisha tiketi kuzongwa au kutakiwa kutoa ufafanuzi ni pamoja na
abiria kupewa tiketi za wanafunzi wakati wamelipa nauli ya watu wazima.
Baadhi
ya abiria walijikuta wakikata tiketi nyingine kutokana na za awali
kuisha muda wake. Hali hiyo ilitokana na wakazi hao kukata tiketi na
kwenda kwenye shughuli zao nyingine na walipofika kituoni na kukuta muda
wake umeisha walilazimika kukata nyingine.
“Awali
walisema hizi tiketi unaweza kupandia basi wakati wowote lakini
nashangaa leo nimekata tiketi nikaamua kwenda kwenye shughuli nyingine.
Nimerudi hapa wakati tiketi inakaguliwa ikagoma kusoma kwa madai kuwa
muda wake wa matumizi umeisha,” alisema mmoja wa wakazi wa Kimara Mwisho.
Akijibu
hoja hiyo, Mgwasa alisema tiketi za karatasi zinatakiwa kutumika kwa
safari moja na kuwa zinadumu kwa saa mbili kabla ya kuisha muda wa
matumizi na ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kukata tiketi pale tu
wanapotaka kusafiri.
Tiketi
zilizokuwa zikitolewa na mawakala wanaohusika zilikuwa hazina maelezo
ya nauli waliyolipa abiria zaidi ya kuonesha tarehe, muda uliokata,
kituo ulichokatia jambo ambalo liliwafanya abiria kuhoji na kuona ni
ujanja wa kupoteza mapato ya serikali.
Note: Only a member of this blog may post a comment.