NI Jumamosi nyingine mpenzi msomaji tunakutana kwenye uwanja wetu wa kupeana mada mbalimbali zenye ujumbe wa masuala ya uhusiano na ndoa.
Ni ukweli usiopingika kwamba siku hizi ndoa nyingi hazidumu. Watu wanaoana kwa mbwembwe nyingi lakini ndani ya miezi kadhaa, mwaka mmoja au miwili, wanaachana. Ukifanya utafiti wa kina utakutana na sababu mbalimbali zinazosababisha tatizo hilo.Ukirudi katika historia utagundua kwamba, kizazi kile cha ndoa zilizofungwa miaka ya tisini kurudi nyuma, kilikuwa tofauti. Ndoa zilifungwa na kudumu kwelikweli.
Suala la msingi hapa la kujiuliza ni kwa nini ndoa za sasa hazidumu?
Zipo sababu nyingi zinazosababisha tatizo hilo lakini kwenye makala haya tutazijadili chache ili mwisho wa siku kila mmoja wetu, aangalie kitu cha kufanya ili kuhakikisha anaingia kwenye ndoa salama na itakayodumu.
Utandawazi
Utandawazi ni suala ambalo kwa kiasi kikubwa limechangia kuharibu maadili ya Watanzania wengi wamekuwa wakiiga maadili ya nchi za Magharibi na kuyaweka katika mazingira ya ndoa zetu. Mfano; mtu anafuata utamaduni ambao pengine unaruhusu mapenzi ya jinsi moja.
Anapokutana na mwenzake ambaye utamaduni huo hakubaliani nao, moja kwa moja ndoa yao itakuwa na migogoro ambayo mwisho wa siku huishia kuvunjika. Pia kutokana na utandawazi huo, watu wamegeuza ndoa kuwa ni kama fasheni.
Kwamba anaweza akaoa leo, kesho akaachana na mwenzake. Anaweza akaoa tena kulingana na mahitaji yake kwa wakati huo. Hachukulii kwa uzito suala la ndoa akiamini kwamba hata akiachana na mkewe, hawezi kuwa wa kwanza. Wengi tu wameshaachana.
Maadili
Kizazi cha sasa kimepotoka kimaadili. Wengi wanafikiri ujanja ni kuishi kama wenzetu Wazungu. Wanawake na wanaume wanaamini kuvaa nguo za ‘mitego’ ndiyo chambo cha kunasa wapenzi.
Mwanamke anaolewa lakini bado anataka atamaniwe na watu. Anajirahisisha bila hofu kwamba utayari wake unaweza kusababisha maafa katika ndoa.
Yupo tayari tu ndoa ivunjike. Anaona hakuna cha kupoteza. Anaamini yeye ni bidhaa adimu. Inayoweza kuuzika wakati wowote. Kwamba anaweza kuachwa, ndani ya muda mfupi atapata ‘mteja’ mwingine ambaye ataendeleza jahazi la mahitaji ya ndoa.
Hofu ya Mungu
Kizazi cha sasa kimemsahau Mungu. Hakina hofu ya Mungu. Suala hili limechangiwa pia na wazazi. Wameshindwa kuwajengea misingi imara katika ngazi ya chini matokeo yake wanawashindwa.
Mzazi anaweza kuwa na maadili mazuri, anakwenda msikitini au kanisani, ana hofu ya Mungu lakini mtoto wake hana.
Tamaa
Kizazi cha sasa kimeharibiwa na utandawazi. Mtu anaingia kwenye ndoa si kwa sababu ya mapenzi ya dhati. Anaongozwa na tamaa ya mwili. Matokeo yake anakutana na mtu ambaye si sahihi. Wataingia kwenye ndoa, watajikuta wanagombana na baadaye wanaachana.
Nini kifanyike?
Kwa yeyote anayetaka kuingia kwenye ndoa anapaswa kuingia bila tamaa za kimwili. Aangalie tabia njema ya mwenzake. Aaangalie kama mwenzake ana hofu ya Mungu.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.
Note: Only a member of this blog may post a comment.